JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUIMARIKA KWA MFUMO WA KUDHIBITI FEDHA HARAMU
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Fedha Haramu (The Eastern and Southern Africa Anti - Money Laundering Group (ESAAMLG)) ulioanzishwa mwaka 1999, kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Baada ya kuanzishwa kwa umoja huo, Tanzania ilitunga Sheria za Kudhibiti Fedha Haramu mwaka 2006.
Umoja wa ESAAMLG umejiwekea utaratibu wa kufanya tathmini ya mifumo yao ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa kuzingatia mazingira ya nchi wanachama na viwango vya kimataifa vilivyowekwa na kikosi kazi cha kimataifa kijulikanacho kama "The Financial Action Task Force "(FATF)".
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanyiwa tathmini ya mfumo wake wa kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi mwaka 2009. Tathmini hii ilihusu maeneo ya kisheria, sera na kitaasisi. Aidha, mkutano wa FATF uliofanyika mwezi Juni, 2014 mjini Paris - Ufaransa, ulijadili hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Tanzania na kuridhika kuwa hatua hizo ni kubwa na endelevu na kuwa ipo dhamira ya hali ya juu ya kisiasa katika kuimarisha mfumo wa kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi nchini.
Pamoja na hatua hizi muhimu za kuimarisha mfumo wa kudhibiti fedha haramu na uhalifu kwa ujumla, Kitengo chetu cha Kudhibiti Fedha Haramu kimekua mwanachama wa umoja wa vitengo vya kudhibiti fedha haramu duniani unaojulikana kama "Egmont Group of Financial Intelligence Units". Kujiunga na umoja huu kutakiwezesha kitengo cha kudhibiti Fedha Haramu Tanzania kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoshughulikia udhibiti wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi duniani, kurahisisha kupata taarifa za kiintelijensia zinazotakiwa katika utendaji wake wa kazi na kuongeza weledi na tija ya utendaji kazi kupitia mafunzo maalum na ubadilishanaji utaalam baina ya vitengo vya udhibiti wa fedha haramu.
Kutokana na hatua zote hizi, tunapenda kuujulisha umma kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingizwa katika orodha ya nchi zenye mifumo imara ya Kudhibiti Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi na hivyo tutaendelea kuimarisha na kusimamia mfumo wetu kwa manufaa na usalama wa mali za wananchi wetu.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila fedha haramu wala uhalifu inawezekana!!
Taarifa hii imetolewa na
Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha
11468 Dar Es Salaam