Na Sultani Kipingo
Habari zilizotufikia sasa hivi zinasema kuwa Bi Julia Pierson (pichani) , Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Rais wa Marekani maarufu kama Secret Service, amejiuzuru nafasi hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wan chi hiyo Bw. Jeh Johnson ametangaza leo. Katika taarifa yake Bw. Johnson kasema atamteua Bw. Joseph Clancy kukaimu wadhifa huo nyeti.
Afisa habari wa Ikulu ya Marekani Bw. Josh Earnest amesema katika mkutano na wanahabari leo kuwa Rais Barack Obama alimwita Bi Pierson na kumshukuru kwa utumishi wake katika Idara hiyo na nchi ya Marekani, na kwamba Rais huyo aliweka bayana kwamba iko haja ya kuwa na uongozi mpya katika Idara hiyo.
Akiongea baada ya uamuzi huo wa kuachia ngazi, Bi. Pierson alisema ulikuwa ni uamuzi mchungu. "Nadhani (uamuzi huo) kwa maslahi ya Secret Service na umma wa Wamarekani. Congress (Bunge) limepoteza imani name kuongoza Idara hii. Vyombo vya habari navyo vimeweka bayana kuwa hili ndilo wanalotarajia. Ni uchungu kuacha kazi katika Idara hii ambayo inaandamwa na kashfa mbalimbali za uwajibikaji mbovu wa usalama".
Bi Pierson alikuwa amekalia kuti kavu na kuwekwa katika hali ngumu kufuatia matukio kadhaa ya kuhatarisha usalama (wa Rais), ikiwa ni pamoja na mtu mmoja kuruka uzio wa White House na kuingia ndani akiwa na kisu mkononi mnamo Septemba 19 mwaka huu. Inaripotiwa kuwa aliingia humo ndani baada ya kumzidi nguvu afisa usalama aliyekuwa lindo, kabla ya kuzidiwa nguvu na afisa mwingine aliyekuwa amemaliza zamu.
Baada ya tukio hilo, matukio mengine ya kuhatarisha usalama wa Rais yakaibuka. Moja likiwa ni kuruhusiwa kwa mtu mmoja aliyewahi kufungwa jela kuingia katika lifti moja na Rais Obama alipokuwa akizuru Taasisi ya kuzuia magonjwa mwezi uliopita. Pia kuna tukio la mtu kupiga risasi Ikulu hiyo ya Marekani ambayo pia ni makazi rasmi ya Rais wa Marekani.
Jumanne iliyopita Bi Pierson aliwekwa kitimoto na kamati ya Bunge kuhusu matukio hayo. Alisema tukio la karibuni lilikuwa halikubaliki na akakiri udhaifu wa idara katika majukumu yake. "Nakubali kubeba lawama zote", alisema. "Haitotokea tena.