Wednesday, October 01, 2014

Timu ya Wizara ya Habari yawatunishia misuli Hazina.




Timu ya Wizara ya Habari yawatunishia misuli Hazina.
 Na Eleuteri Mangi-MAELEZO 
Mji wa Morogoro na viunga vyake imepambwa kwa shamra shamra za mashindano ya Shirikisho la Michezo ya watumishi Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea katika viwanja mbalimbali mjini hapo. 
Kwa kipindi cha wiki mbili, watumishi wamekuwa wakionesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, mpira wa pete na michezo ya ndani. 
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo ndio Wizara yenye dhamana ya michezo imedhihirisha ukakakamavu wake katika mashindano hayo leo mjini Morogoro. Ikiwa na timu mahiri, wizara hiyi imeibuka kidedea katika mchezo wa kuvuta kamba kwa timu ya wanawake na ya wanaume dhidi ya wapinzani wao Hazina kwa kuwavuta kwa mizunguko yote miwili kwa timu zote mbili. 
Kazi ya kuvuta kamba haikuwa ngumu kwa timu za Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwani hikuwachukua muda mrefu kuwavuta wapinzani wao hata kabla ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo. Ikumbukwe kuwa michezo ya SHIMIWI imekuwa ni sehemu ya wafanyakazi ambao ni watumishi wa umma kupata fursa ya kujenga afya zao kwa kuwa michezi ni afya kwa maendeleo ya mtumishi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. 
Zaidi ya hayo, michezo ya SHIMIWI imekuwa desturi ya kujenga udugu, amani upendo na mshikamano kati ya wachezaji na viongozi wa michezo husika katika jamii. Aidha, katika mpira wa pete, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imetoka suluhu kwa kutoa sare na timu ya Ulinzi kwa kufungana kwa magoli 18 kabla ya mechi za mwisho za hatua ya makundi ambayo inatarajiwa kumalizika siku ya Alhamisi Oktoba 2 mwaka huu. 
Mashindano hayo yanayoendelea mjini Morogoro yanafanyika katika viwanja vya Jamhuri, Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Mazimbu na chuo cha Ujenzi ili kutoa mwanya wa michezo mingi kufanyika kwa mara moja.  
 Picha ya pamoja ya timu ya kuvuta kamba wanawake kabla ya mechi ya kuvuta kamba na timu ya Hazina  ambapo walishinda kwa kuwavuta kwa 2-0
 Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu wa timu ya Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mchezo wao na timu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii leo mjini Morogoro.

 Wachezaji wa mpira wa pete timu ya Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo wakiwa katika pozi kabla ya kuanza mechi yao na timu ya Jeshi la Ulinzi
 Timu ya kuvuta kamba ya wanaume ya Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo iliyowatoa jasho timu ya Hazina kwa kuwavuta kwa 2-0 wakati wa mashindano ya SHIMIWI mjini Morogoro.

Timu ya kuvuta kamba ya wanawake ya Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo ikionesha umahiri wao wakati wa mashindano ya SHIMIWI mjini Morogoro ambapo walishinda timu ya Hazina kwa kuwavuta kwa 2-0