Monday, October 06, 2014

BREAKING NEWZZZZZ: Dkt. William Ferdinand Shija afariki dunia



BREAKING NEWZZZZZ: Dkt. William Ferdinand Shija afariki dunia
Sekretarieti ya CPA Kanda ya Afrika inasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, (CPA) Dkt. William Ferdinand Shija (pichani) kilichotokea katika Hospitali ya Charring Cross, London Uingereza tarehe 4 Oktoba, 2014.

Taarifa ya kifo chake imekuja wakati ambapo Mkutano wa 60 wa CPA unafanyika Yaoundé, Cameroon.

Dkt. William Shija amefanya kazi kwa takriban miaka 8 kama Katibu Mkuu wa Chama cha Wabunge wa Jumuiya ya Madola. Amefanya kazi kubwa kwa CPA na ameacha rekodi kubwa ya utendaji wa kazi akiwa pia ndio Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika katika Chama hicho.

Katika uhai wake, Dkt. William Shija amefanya kazi ikiwa ni pamoja na kushikilia nyadhifa zifuatazo katika Serikali ya Tanzania:-

§  Waziri wa Viwanda na Biashara;
§  Waziri wa Nishati na Madini;
§  Waziri wa Habari na Utangazaji
§  Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu; na
§  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Aidha, Dkt. William Shija amekuwa Mbunge kwa takriban miaka 15. Akiwa Mbunge, Dkt. William Shija alikuwa Mwenyekiti na Mjumbe katika Kamati zifuatazo:-
§  Mambo ya Nje; na
§  Habari; Utamaduni na Utalii.

Vile vile, amewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika ambapo aliongoza Timu ya Uangalizi wa Uchaguzi kutoka Bunge hilo kwa Uchaguzi Mkuu wa Malawi mwaka 2004.

Kitaaluma, Dkt. Shija amesoma na kuhitimu Shahada za Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Howard Nchini Marekani. Alisoma na kuhitimu Shahada ya kwanza na Stashahada ya Uandishi katika Chuo Kikuu cha New Delhi. Amefanya kazi kama Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Nyegezi na pia amewahi kufundisha katika Chuo cha Utumishi wa Umma na Chuo cha Uhazili Tabora.

Dkt. Shija ameacha Mke Bibi Getruda Peter Shija na watoto watano; Leo, Anna, George, Ferdinand na Monica.

Sekretarieti ya CPA kwa kushirikiana na Familia ya marehemu, Bunge la Tanzania, Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na Mwajiri wake CPA Makao Makuu na CPA Makao Makuu inaratibu mazishi yake ambapo mwili wa marehemu utawasili nchini tarehe 11 Oktoba, 2014 na kuagwa rasmi katika Viwanja vya Karimjee siku ya Jumapili tarehe 12 Oktoba, 2014 kabla ya kusafirishwa kuelekea Sengerema kwa mazishi.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi;

AMINA
                                         
Dkt. Thomas Didimu Kashililah
KATIBU WA CPA KANDA YA AFRIKA