Wafanyakazi wa Benki ya Exim tawi la Mwanza na wawakilishi wa gereza la Butimba wakiwa katika picha ya pamoja, muda mfupi baada ya Benki hiyo kukabidhi vifaa vya usafi kwa gereza la Butimba lililopo jijini Mwanza hivi karibuni. Mchango huo ni sehemu ya shughuli za kibenki za kijamii lakini pia ukilenga kusaidia wafungwa kubadili tabia.
Exim Bank imeahidi kuendelea kusaidia juhudi za serikali katika kuboresha hali ya magereza nchini, ikiwa ni sehemu ya shughuli zake za kibenki za kijamii. Benki iyo imekabidhi vifaa vya usafi kwa wanawake wanaotumikia vifungo katika gereza la Butimba jijini Mwanza, hatua inayolenga kuwasaidia na kuwaelimisha wanawake hao kubadili tabia.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika katika gereza la Butimba jijini Mwanza hapo jana, Mkuu wa Matawi wa Benki ya Exim Mwanza, Bw. Justus Mukuras alisema mchango huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa wafungwa walio katika gereza hilo. Alisema mbali na mchango wa vifaa hivyo, benki hiyo iliajiri mwanasaikolojia ambaye alizungumza na wanawake hao na kuwapa faraja pamoja na kuwafundisha mbinu mbalimbali za maisha. Lengo likiwa kuwafanya kuwa mfano bora katika jamii zao pindi watakaporudi uraiani.
"Hii ni sehemu ya shughuli zetu za kijamii na hatulengi kuishia hapa, hizi ni jitihada endelevu zilizo chini ya kampeni ya benki yetu ya kusaidia wafungwa wa kike nchini. "Pamoja na mambo mengine, kampeni hiyo inalenga kuwafundisha wafungwa mbinu mbalimbali za maisha na kuwafanya wawe watu bora zaidi. Tutaendelea kuwasaidia vifaa vya usafi pamoja na vifaa vingine kwa watoto wanaoishi na mama zao katika magereza," alisema Bw. Mukuras.
Wafungwa wengi nchini wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya usafi pamoja na vyakula; hii inatokana na idadi kubwa ya wafungwa katika magereza hali inayopelekea mlipuko wa magonjwa.
"Sisi kama benki tungependa kutekeleza jukumu letu la kusaidia jamii hususani wanawake wanaotumikia vifungo katika magereza pamoja na watoto wanaoishi na mama zao katika magereza hayo kwani baadhi yao wanakabiliwa na upungufu wa virutubisho na afya duni. Ukipata nafasi ya kuingia katika magereza ndipo utakapobaini idadi ya matatizo wanayokumbana nayo," aliongeza Bw. Mukuras.