Baadhi ya waandishi wa habari wanaosafiri kwenda Malawi wakiwa wanamsikiliza Katibu tawala msaidizi wakati wa kuagana.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha akizungumza na waandishi wa Habari wanaotarajia kusafiri.
Mwenyekiti wa safari ya Malawi, Ulimboka Mwakilili, akitoa ufafanuzi wakati wa kuagana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Mwandishi Christopher Nyenyembe, mmoja wa Waandishi wanaosafiri akifafanua jambo.
Katibu tawala Msaidizi akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji Akiongea na Waandishi wa Habari wanaokwenda Safarini Malawi
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, akiwasikiliza waandishi wa habari walipoenda kumuaga ofisini kwake.
baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa ofisini kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wakimsikiliza kwa makini walipoenda kumuaga tayari kwa safari ya Malawi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wanaotarajia kusafiri baada ya kuagana.
BAADHI ya Waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wanaotarajia kufanya ziara ya kimafunzo nchini Malawi na Zambia wameagwa rasmi na viongozi wa Serikali.
Waandishi hao wapatao 15 wanatarajia kuanza safari Septemba 14, Mwaka huu hivyo kabla ya kuondoka wameagana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Maagano hayo yamefanyika leo kwa nyakati tofauti na kupata Baraka zote kutoka kwa wawakilishi wa Ofisi hizo na kuwataka waandishi kuuwakilisha vema Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.
Katibu Tawala Msaidizi, idara ya Utawala na rasilimali watu, Leonard Magacha, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, alisema matarajio ya Mkoa ni kupata mrejesho kutoka kwa waandishi baada ya kurudi kutoka safarini.
Alisema hiyo ni fursa pekee ambayo waandishi wanaitumia kuvitangaza vivutio mbali mbali vilivyopo katika Mkoa wa Mbeya kwa watu wa Malawi ili waweze kutembelea pamoja na fursa zilizopo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, amewataka waandishi wa habari kutumia nafasi hiyo kuitangaza timu ya Mbeya City kimataifa zaidi.
Alisema hivi sasa Halmashauri imekuwa na mahusiano mazuri na wananchi kutokana na uwepo wa timu ya mpira wa miguu ambayo hivi sasa inajulikana nchi nzima hivyo ni fursa iliyotokea ya kuitangaza nchi za Nje ili ijulikane kimataifa zaidi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Msafara wa Waandishi wa Habari kwenda nchini Malawi, Ulimboka Mwakilili, ametoa shukrani kwa wadau mbali mbali waliowezesha safari hiyo kwa hali na mali.
Alisema mbali na kila mwandishi kuchangia gharama za kwenda na kurudi lakini kuna wadau walioweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya safari hiyo.
Aliwataja baadhi ya wadau kuwa ni Mkurugenzi wa Hifadhi ya wanyama pori(Ifisi Zoo), Leirner, WYCS, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ofisi ya Katibu tawala Mkoa wa Mbeya, Faraja nursing na Maridadi Shop.
Aliongeza kuwa wadau wengine wanakaribishwa kuchangia safari hiyo kutokana na umuhimu wake katika kutangaza fursa ambazo zinapatikana katika Mkoa wa Mbeya kwa wafanyabiashara na wananchi wa Nchi ya Malawi.
Naye Mratibu wa Safari hiyo, Venance Matinya, alisema maandalizi ya safari yamekamilika kwa asilimia kubwa hivyo kinachosubiriwa ni tarehe ya kuondoka.
Alisema waandishi wa habari wameshaajiandaa kwa mahitaji yote ya safari za nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kukata Hati za kudumu za kusafiria pamoja na cheti cha chanjo ya ugonjwa wa manjano kwa mujibu wa sheria.