Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta na Ali Juma Mkangala ,mmoja washiriki wa Mkutano wa Kutatua mgogoro wa kiwanda cha chai cha Liponda kilichopo Bumbuli Tanga.Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Septemba 13, 2014.
Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi (kushoto) na Mbunge wa Bumbuli , Januari Makamba (kulia) wakiteta na Waziri wa Kilimo , Chakula na Ushiriki Mhandisi Christopher Chiza katika mkutano wa kutatua mgogoro wa kiwanda cha chai cha Liponde kilichopo Bumbuli Tanga kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga, Septemba 13, 2014. Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
*Ataka iundwe timu ya watu wachache kusimamia kiwanda
*Amtaka mwekezaji kukubali kufanya kazi na timu ya Serikali
*Asema dawa ni CAG kufanya ukaguzi ili kupata picha halisi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai pamoja na Bodi ya Chai nchini waangalie uwezekano wa kuunda timu ya watu wawili au watatu itakayosimamia mwenendo wa kiwanda cha chai Mponde, kilichopo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili jijini Tanga jana asubuhi (Jumamosi, Septemba 13, 2014) akitokea Dodoma, alipokea taarifa fupi ya mgogoro wa kiwanda hicho kabla ya kuzungumza na wakulima, wadau wa zao la chai na viongozi wa mkoa na wizara kadhaa kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
"Wakala wa Wakulima pamoja na Bodi ya Chai itabidi watusaidie kuunda timu kwa sababu tunahitaji kuwa na jicho la Serikali ndani ya kiwanda… tunahitaji watu wenye uzoefu mkubwa na mambo ya chai ili wasimamie uendeshaji wa kiwanda pindi kitakapoanza kazi," alisema.
"Vilevile mwekezaji itabidi akubali kufanya kazi na timu ya Serikali ili tuweze kujua kwa leo kiwanda kiko katika hali gani na tukitaka kukifungua ni lazima tufanye nini," aliongeza.
Waziri Mkuu alisema timu hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji hawana budi kuandaa mpango-kazi wa miaka miwili hadi mitatu wa kufufua kiwanda ili uzalishaji wa chai ufikie pazuri. "Kiwanda wakati kinabinafsishwa kilikuwa na uwezo wa kusindika kilo 20,000 za majani ya chai lakini kilikarabatiwa na kufikisha uwezo wa kusindika kilo 120,000 kwa siku. Sasa tuangalie uwezekano wa kuongeza uzalishaji kwani hapo tutaweza pia kuongeza mavuno kwa wakulima wetu," alisema.
Alisema ili kuweza kusonga mbele, itabidi Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aende kufanya ukaguzi kwenye kiwanda hicho ili kuweza kutoa picha halisi ya kiwanda hicho kwa sababu Serikali ina hisa.
Kiwanda cha Chai cha Mponde kinamilikiwa na Chama cha Wakulima wa Chai cha UTEGA (Usambara Tea Growers Association) ambacho kilitafuta mwekezaji ambayo ni Kampuni ya Chai ya Lushoto (Lushoto Tea Company). Wakulima wa Chai walikifungia kiwanda hicho kisifanye kazi kwa madai kuwa walikuwa hawalipwi walipo kwa wakati, wamiliki kutumia lugha chafu,Baada ya kusikiliza pande zote, Waziri Mkuu alikubaliana na rai iliyotolewa na pande hizo kwamba kuna haja ya kufungua kiwanda hicho ambacho kilifungwa tangu Mei 26, 2013 ili kuwasadia wakulima wapate soko la chai lakini pia waweze kujikimu mahitaji yao.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi Chiku Gallawa alisema mkoa wa Tanga ulijipanga kukuza kiwango cha ukusanyaji mapato ili kuendana na mpango wa Serikali wa matokeo makubwa sasa lakini kufungwa kwa kiwanda hicho, kumeshusha pato la mtu mmoja mmoja, pato la mkoa na pato la Taifa kwa ujumla.
"Changamoto kubwa ambayo tumekabiliana nayo kwa kipindi chote hiki ambacho kiwanda kilikuwa kimefungwa, ni kwa wananchi kushindwa kuuza chai yao," aliongeza.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw. Majjid Mwanga akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu alisema kiwanda cha Mponde kilikuwa na uwezo wa kusindika kilo 70,000 za majani mabichi ya chai kwa siku lakini hadi kinafungwa uwezo huo ulishuka na kufikia kilo 25,000 kwa siku.
Alisema idadi ya wakulima walioathirika kutokana na kufungwa kwa kiwanda hicho ni 3,908 ambao walikuwa wakilima hekta 1,951. "Bei ya kilo moja ya chai ilikuwa ni sh. 225/- wakati wastani wa pato la mkulima kwa nusu hekta ilikuwa ni sh. 180,000/- kwa mwezi lakini kwa sasa limeshuka na kufikia sh. 90,000/- kwa mwezi kwa nusu hekta hiyo hiyo," alisema.
Alisema zaidi ya tani 1,800 zimeshindikana kusindikwa na hivyo kuikosesha Halmashauri yao kiasi cha sh. milioni 21.6/- ambazo zilikuwa zikilipwa kama ushuru kwa kila kilo moja iliyokuwa ikiuzwa. "Wakulima kwa ujumla wao wamepata hasara ya sh. milioni 370.8/-" alisema.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa pia na Mawaziri wa OWM-TAMISEMI; Kilimo, Chakula na Ushirika; Viwanda na Biashara, Wabunge wa Mlalo, Bumbuli na Lushoto; viongozi wa Mkoa na Halmashauri za Korogwe, Lushoto na Bumbuli, viongozi wa UTEGA na mwekezaji, ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha Lushoto Tea Company.
IMETOLEWA NA :
OFISI YA WAZIRI MKUU
S.L.P 3021
DAR ES SALAAM
JUMAPILI,SEPTEMBA 14.2014
IMETOLEWA NA :
OFISI YA WAZIRI MKUU
S.L.P 3021
DAR ES SALAAM
JUMAPILI,SEPTEMBA 14.2014