"PIGA KITABU NA LAPF"
WANACHAMA WA LAPF KUNUFAIKA NA FAO LA ELIMU
Bilioni 3 kutumika mwaka wa masomo 2014 – 2015 kutoka mfuko wa pensheni wa LAPF kwa wanachama wake.
15 Septemba 2014, Dodoma: Wanachama wa mfuko wa penseni wa LAPF kunufaika na fao jipya lilozinduliwa hivi karibuni nchini kwa Baraka zake Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Mh. Hawa Ghasia.
Fao hilo lijulikanalo kama 'Piga Kitabu na LAPF' limelenga kuwakopesha wanachama wa LAPF mikopo ya elimu ya juu kwani ni ombi la muda mrefu kutoka kwa wanachama wa mfuko huo. Hivyo kwa kuthamini na kuona umuhimu wa elimu Mfuko wa Penseni wa LAPF umjibu kiu yao ya muda mrefu ili kumpunguzia mzigo mwajiri.
Akiongea kutoka Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa LAPF Bwana Eliud Sanga alieleza kuwa mfuko wa Pensheni wa LAPF una huduma nyingi na ambazo zimelengwa kwa ajili ya jamii na hususani zinazochangia sana kwenye maendeleo.
"Huduma hii mpya ya Fao la Elimu imetengewa shilingi Bilioni Tatu (3) kwa mwaka huu wa fedha ikiwa ni kianzio cha mfuko huu, tunaahidi mwaka unaofuata fao hili litatengewa bajeti kubwa zaidi kutokana na umuhimu wake katika nchi yetu, wanachama wengi wameshanufaika mpaka sasa na wengine wengi zaidi wanazidi kutuma maombi ya kupata mkopo wa elimu ya juu. Fao hili litawanufaisha wanachama maelfu na maelfu, wanachama wengi watume maombi kunufaika na huduma hii"
"Mwanachama anatakiwa kujaza fomu ya mkopo wa elimu LAPF/LON.2, ambayo hupatikana katika ofisi zote za LAPF pamoja na ofisi za waajiri wachangiaji na pia kwenye tovuti ya LAPF www.lapf.or.tz. Baada ya kukamilisha fomu na kuambatisha vielelezo vinavyotakiwa atawasilisha fomu hiyo kwenye ofisi za LAPF au atatuma kwa njia ya posta. Fao hili la Mkopo wa Elimu kwa mwanachama utalipwa moja kwa moja chuoni kila mwaka wa masomo kwa taratibu za chuo husika na urejeshaji wake utakuwa kwa muda wa miaka mitano tangu ulipoanza kutolewa" Aliongeza Bwana Sanga.
'Piga Kitabu na LAPF' ni fao la elimu litakalotolewa kwa mwanachama yoyote wa lapf ambaye amekidhi vigezo kama kupata kibali cha kusoma toka kwa mwajiri wake, barua (admission letter) ya kukubalika kujiunga na chuo cha hapa nchini kilichosajiliwa na nacte au tcu na awa na michango inayozidi kiasi cha mkopo unachoombwa kwa asilimia 25.