Na Greyson Mwase, Bagamoyo
Jumla ya Dola za Marekani milioni 53.8 zilipatikana kutokana na mauzo ya vito mbalimbali ndani ya nchi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchambuzi na Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito, (TANSORT) kilichopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini Archard Kalugendo kwenye semina iliyoshirikisha Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Afisa Madini Wakazi na Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini inayoendelea Bagamoyo yenye lengo la kujadili utendaji na uboreshaji wa shughuli za uthaminishaji wa madini ya almasi na vito nchini.
Kalugendo alisema kuwa mauzo hayo yanatokana na usimamizi mzuri wa Kitengo hicho katika kuthaminisha almasi na vito kwa ajili ya kukokotoa mrabaha wa Serikali; Kutayarisha miongozo ya bei (Price Guides) ya almasi na madini ya vito inayotumika kukokotoa mrabaha na Kutoa huduma za kijemolojia (Gemmological Services) kwa wachimbaji wadogo na wa kati na Kusimamia mauzo na kufuatilia mwenendo wa masoko ya almasi na madini ya vito.
" Kutokana na usimamizi mzuri wa mauzo na kufuatilia mwenendo wa masoko ya almasi na mad ini ya vito, ulipelekea wastani wa bei ya almasi za Tanzania katika soko la dunia kupanda hadi dola za Marekani 286 kwa karati ikiwa ni ongezeko la asilimia 13, alisisitiza Kalugendo
Alisema masoko saba ya kimataifa yalifatiishwa ili kutambua mwenendo wa bei na masoko ya madini ya vito na almasi duniani ambayo ni Bangkok, Antwerp, Basel, London, Changsha, Las Vegas na Arusha.
Kalugendo aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na usimamizi mzuri wa shughuli za uthamini wa almasi na madini ya vito ni pamoja na mauzo ya Tanzanite kuliingizia Shirika la Madini la Taifa (Kalugendo aliainisha mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni pamoja na Kilo 818, gramu 269,211 na carat 40,599 za Tanzanite kuthaminiwa na kuuzwa na mgodi wa TanzaniteOne Minerals Limited (TML) wa Arusha.
Akielezea changamoto za TANSORT Kalugendo alisema ni pamoja na kada ya Wajemolojia kutokuwa katika muundo wa Kada za Utumishi wa Umma , kutokuwepo kwa kituo maalum cha kufanyia biashara ya almasi na vito nchini na kuendelea kwa vitendo vya wizi, udanganyifu, utapeli na utoroshwaji wa madini ya almasi na vito nchini.
Kalugendo aliendelea kueleza kuwa kumekuwepo a ukwepaji wa kodi na tozo za Serikali miongoni mwa wazalishaji na wafanyabiashara wadogo wa almasi na vito hali inayopelekea taifa kukosa mapato yake stahiki.
Akielezea mikakati katika utatuzi wa changamoto hizo Kalugendo alisema rasimu ya Kada ya Wajemolojia imekamilika kwa ajili ya taratibu zinazofuata pamoja na matayarisho kwa ajili ya soko rasmi la kuuzia madini ya thamani kubwa hapa nchini kuendelea kufanyiwa kazi na Wizara.
Alisema hatua mbalimbali zinazoendelea ni pamoja na kufanya tathmini za mapato, kutafuta uwekezaji katika jengo hilo, kutathmini namna bora ya kuendesha soko hilo na kujifunza kutoka nchi nyingine juu ya uendeshaji bora wa masoko ya jinsi hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa TANSORT imejipanga kuendelea kutoa elimu juu ya athari za vitendo vya udanganyifu, wizi, ukwepaji kodi, na utoroshaji wa madini ya vito.
TANSORT ni Kitengo cha Uchambuzi na Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini ambapo uthamini unalenga ukokotoaji sahihi wa mrabaha wa Serikali kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Vifungu vya 87, 88 na 89. Kitengo hiki kilichoanzishwa mwaka 1966 kina ofisi tano sehemu tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na Antwerp nchini Ubeljiji, Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam) Kanda ya Kati- Magharibi (Shinyanga) Kanda ya Kaskazini (Arusha) Kanda ya Kusini (Songea).