Wizara ya Ujenzi napenda kutoa taarifa ka umma kuwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (Mb) anatarajia kufanya ziara ya kukagua miradi mbaimbali ya Maendeleo katika mkoa wa Mwanza na Mara.
Mheshimiwa Waziri Magufuli ataanza ziara yake Mkoani Mwanza tarehe 06 Julai ambapo atakagua mradi wa Ujenzi wa barabara ya Usagara – Kisesa (by pass) yenye urefu wa km. 16.7 inayojenga kwa kiwango cha lami.
Siku inayofata tarehe 07 Julai, Mheshimiwa Waziri ataelekea mkoani Mara kukagua mradi wa barabara ya Makutano – Natta – Mugumu (sehemu ya Makutano – Sanzate km 50).
Siku hiyo hiyo mchana Dkt. Magufuli atazindua rasmi kivuko cha MV. Mara kitakachotoa huduma kati ya Iramba na Majita.
Aidha, baada ya uzinduzi huo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi atafanya mkutano wa hadhara na kuongea na wananchi wa eneo la Mwibara ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa mradi wa Barabara ya Nyamuswa – Bunda – Kisorya – Nansio (sehemu ya Bulamba – Kisorya km 51).
Mheshimiwa Magufuli ataendelea na ziara yake tarehe 09 Julai Mkoani Mwanza ambapo atazindua kivuko cha MV. Temesa katika eneo la Nyegezi(Sweya).
Kivuko hicho kimefungwa mitambo ya kukiwezesha kusafiri kwa mwendo wa kasi ili kukiwezesha kutoa huduma katika mwambao huo wa ziwa Victoria. Aidha, Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba Tani 65 ambazo ni sawa na abiria 80 na magari madogo matano kwa wakati mmoja.
Kivuko hicho kitakuwa kinafanya kazi kutoka Luchelele kupitia Sweya, Butimba, Mkuyuni, Igogo hadi Kirumba ikiwa ni mkakati wa kupunguza foleni katika jiji la Mwanza.
NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI
05/07/2014