Waziri wa Ujenzi Dkt.John Magufuli ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kutopakia magari ndani ya kivuko kipya cha MV TEMESA ili kibebe wananchi wengi zaidi katika mwambao wa ziwa Victoria.
Dkt.Magufuli alitoa agizo hilo katika kijiji cha Swea nje kidogo ya jiji la Mwanza wakati akikizindua kivuko hicho kitakachokuwa kinatoka Luchelele hadi mjini huku kikipitia katika vituo mbalimbali vitakavyowekwa. Waziri Magufuli alisema kuwa agizo hilo la kutobeba magari litasaidia kuongeza idadi ya watu ndani ya kivuko hicho.
Kuhusu muundo wa Kivuko hicho, Dkt. Magufuli alisemaa kwamba Mv TEMESA kimefungwa mitambo ya kukiwezesha kusafiri kwa mwendo wa kasi ili kukiwezesha kutoa huduma kwa haraka na ufanisi katika mwambao huo wa ziwa Victoria
Aidha, Waziri Magufuli aliongeza kuwa wakati Kivuko hicho kinajaribiwa katika eneo la Kigongo hadi Busisi, kilitumia muda wa dakika tisa tu wakati Ferry zilizopo hapo zinatumia muda nusu saa kukamilisha safari moja.
"Kivuko hiki kitakuwa cha aina yake kutokana na mwendokasi wake hivyo tunatarajia ndani ya nusu saa kitakuwa kimeshafika mjini kutokea mwanzo wa safari yake"alisema Waziri Magufuli
Kuhusu nauli ya Kivuko hicho, Dkt Magufuli alisema kuwa kwa kila abiria atakayepanda atalipa shilingi 500, na kwa wanafunzi watakaovalia sare watasafiri bure na kwa wale walio chini miaka 18 watalipa shilingi 100 ili kupunguza safari zisizo za msingi.
Pia Waziri Magufuli alitoa agizo kuwa ndani ya wiki moja kivuko hicho kinatakiwa kiwe kimeanza kazi pamoja na kuwepo ratiba ya kueleweka kuanzia asubuhi kwa ajili ya wanafunzi pamoja na wasafiri watakaokuwa wanafanya kazi mjini. Kivuko cha Mv Temesa kina uwezo wa kubeba Tani 65 ambazo ni sawa na abiria 80 na magari madogo matano kwa wakati mmoja.
Kuhusu maombi yaliotolewa na mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Ndikilo pamoja na Mstahiki Meya wa jiji la mwanza Stanslaus Mabula, Dkt. Magufuli alisema ameyapokea na atayafanyia kazi "Kuhusu ombi la Mkuu wa Mkoa la kujenga Daraja la waenda kwa miguu flyover pale Ghana karibu na viwanja vya Furahisha tumelipokea na tutatafuta fedha tulijenge na jiji la mwanza liwe la mfano kwa Africa nzima" alisema Waziri Magufuli
Waziri Magufuli aliongeza kuwa kuhusu barabara za Mawe katika kijiji cha Swea, wizara ya Ujenzi kupitia Fedha za mfuko wa barabara itahakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika na tayari mkoa wa mwanza umetengewa fedha kutoka kwenye mfuko huo wa barabara.
Wananchi wa rika na jinsia zote waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo kama inavyoonekana pichani ambapo Mheshimiwa Waziri Magufuli alizindua kivuko hicho
Kivuko cha MV. Temesa kilichozinduliwa na Mhe. Magufuli kikielea majini mara tu baada ya kuzinduliwa .
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mhandisi Mussa Iyombe katikati akimshuhudia nahodha wakivuko hicho akifanya kazi yake kama inavyoonekana mara tu baada ya uzinduzi.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John Magufuli akikata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa Kivuko cha MV Temesa kitakachotoa huduma katika mwambao mwa Ziwa Victoria kikianzia Luchelele hadi Mjini na kupitia vituo mbalimbali vitakavyowekwa
Wakazi wa jiji la Mwanza waliojotokeza kwa wingi kushuhudia kitendo cha kihistoria kilichofanywa na Mheshimiwa Waziri Magufuli kuzindua kivuko cha kwanza nchini kilichotengenezwa kwa ajili ya kupunguza msongamano ya magari katika jiji la Mwanza.