Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii
WAKAZI wa jijini Dar es Salaam 16 leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi mbili tofauti ikiwemo ikiwemo kula njama na kusaidia wenzao kufanya ugaidi sehemu mbalimbali Tanzania na kutumia mtandao wa Fesibuku kupata mbinu za kutengeza mabomu ya kwenda kufanya ugaidi nchini Kenya.
Katika kesi ya kwanza washtakiwa hao ni, Nassor Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassan maarufu kama Jibaba, Hussein Ally, Juma Juma, Said Ally, Hamis Salum, Said Salum, Abubakar Mngodo, Salum Salum, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange ama Mapala na Amir Juma.
Mashtaka hayo yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa wa mahakama hiyo. Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila akisaidiana na Mawakili wa Serikali, George Barasa, Mwanaamina Kombakono na Brenda Nick.
Barasa alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2013 na mwaka huu sehemu mbalimbali nchini Tanzania, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la kusaidia kufanyika ugaidi. Ilidaiwa katika shitaka la pili, kati ya Januari mwaka 2013 na June mwaka huu sehemu mbalimbali Tanzania, washtakiwa wote kwa pamoja waliwasaidia Sadick Absaloum na Farah Omary kufanya ugaidi kinyume cha sheria.
Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa Julai 23, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu. Katika kesi ya pili, mshtakiwa ni, Jihad Swalehe anakabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo kula njama na kufanya mawasiliano kupitia mtandao wa kijamii Facebook ya kupata mbinu za kufanya ugaidi nchini Kenya. Nick alidai kuwa siku na mahali pasipofahamika jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikuwa na njama ya kutenda kosa la kigaidi.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa kati ya Machi 21, mwaka 2013 na Juni 2, mwaka huu mahali pasipofahamika kupitia mtandao wa Facebook, mshtakiwa alifanya mawasiliano na Nero Saraiva na wengine kumsaidia namna ya kutega mabomu nchini Kenya kwa lengo la kuwasababishia kupoteza maisha na majeraha wananchi wa nchi hiyo.
Washtakiwa wote kwa nyakati tofauti hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Mapema leo katika viunga vya Mahakama ya Kisutu, washtakiwa hao walifikishwa wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari kanzu wenye bunduki na Kikosi Maalum cha kutuliza ghasia (FFU) waliokuwa na silaha pamoja na mabomu.
Hali ilikuwa tulivu huku askari hao wakiimarisha ulinzi kila kona ya viunga hivyo jana saa 6:05 mchana mara tu baada ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo. mwisho