Tuesday, July 08, 2014

Wasafiri wa treni waliokwama Manyoni wasafirishwa kwa mabasi kuja Dar




Wasafiri wa treni waliokwama Manyoni wasafirishwa kwa mabasi kuja Dar
Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania – TRL unawaarifu wananchi kwa jumla kuwa imefanikiwa kuwasafirisha kuja Dar abiria takriban 678 waliokwama katika Stesheni ya Manyoni. Zoezi hilo linaloendeshwa kwa awamu mbili tofauti lilianza usiku wa manane hadi saa 10 usiku wa kuamkia leo .

Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi zoezi la pili litaanza tena kuanzia saa asubuhi ya leo kwa abiria wapatao 699 waliosalia kutegemeana na kupatikana mabasi mengine zaidi ya 11 yanayohitajika.

Kukwama kwa treni hiyo iliyokuwa ikitokea Tabora kuja Dar kumesababishwa na ajali ya treni ya mzigo iliyokuwa ikienda Bara ambapo ilitokea kati ya Stesheni za Kintinku na Makotopora km 539/6-0 jana saa 6:50 mchana. Katika ajali hiyo mabehewa 7 yalianguka na moja liliacha reli.

Tathmini ya Wahandisi wetu ni kuwa kazi ya kukarabati njia itachukua saa 12 na hivyo njia inatarajiwa kufunguliwa saa 6 usiku wa manane leo.

Safari ya abiria kwenda bara ya leo Julai 08, 2014 itaendelea kama ilivyopangwa hata hivyo muda wa kuondoka umesogezwa mbele ambapo itaondoka stesheni ya Dar es Salaam saa 2:30 usiku.

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi 
 Kipallo Aman Kisamfu.
TRL Makao Makuu, 
 Dar es Salaam. 
 Julai 08, 2014