Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu   jalalani, linalodaiwa kufanywa na  Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na   Teknolojia (IMTU) cha Dar es Salaam,  linadaiwa kuandika historia mbaya   nchini.
  Wakati serikali ikiendelea kuchunguza tukio   hilo, ikiwemo kuunda tume nyingine chini ya Wizara ya Afya na Ustawi,   kujiridhisha kabla ya hatua kuchukuliwa,  Baraza la Madaktari limetwishwa   mzigo wa kuhakikisha linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na   kitendo hicho. 
  Imeeleza kwamba katika miaka  yote,   tangu mafunzo ya udaktari yaanze kutolewa nchini, halijawahi kutokea tukio kama   hilo.
  Serikali imetumia nafasi hiyo kuonya vyuo   vingine, kwa kusema  jambo hili ni la kusikitisha, la aina yake katika   historia ya mafunzo ya udaktari tangu yaanze nchini takribani miaka 40 sasa.   
  "Pia tunatoa onyo kwa vyuo vingine, mafunzo   haya tumeanza miaka 40 iliyopita lakini haijawahi kutokea kitu cha aina hii, ni   mara ya kwanza ni jambo la kusikitisha sana," alisema Naibu Waziri wa Wizara ya   Afya na Ustawi, Dk Steven Kebwe.
  Naibu Waziri aliwaambia waandishi wa habari   kuwa kitendo hicho cha kutupa viungo vya binadamu  hadharani,  si   jambo la kawaida, ni la uvunjifu wa haki za kibinadamu.
  Alisema tangu Tanzania ipate uhuru   wake,  haijawahi kutokea tukio kama hilo, ambalo linatia hofu miongoni mwa   wanajamii.
  Katika kile kinachodhihirisha chuo hicho   kung'ang'aniwa, kabla ya kuamua hatua za kuchukua dhidi yake, Wizara hiyo yenye   dhamana ya afya, pia imeunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kuchunguza tukio   hilo. 
  Kamati hiyo ya wizara iliyopewa siku saba   kukamilisha kazi, imeundwa kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda ya   Dar es Salaam, kuchunguza sakata hilo la kutupwa viungo katika maeneo ya Bonde   la Mbweni Mpiji, Bunju jijini Dar es Salaam. 
  Dk Kebwe aliwaambia waandishi wa habari   kwamba kamati hiyo ya wizara itafanya kazi yake kwa siku saba kuanzia juzi.   Inajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi na Wizara   ya Afya na Ustawi.
  Aidha, alisema zipo sheria zinazoelekeza   namna ya kuteketeza miili hiyo baada ya kumalizika kwa kazi yake. 
  "Lakini inasikitisha kuona miili hiyo   ilitelekezwa na watu wanaojua maadili ya kazi ya udaktari," alisema.
  Alisema kwa kuwa madaktari huwa wanakula   viapo baada ya kumaliza mafunzo yao, Baraza la Madaktari nchini linatakiwa   kuhakikisha linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo   hicho.
  Timu iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda   Maalumu ya Dar es Salaam,  imejielekeza kuja na majibu kadhaa,  ikiwa   ni pamoja na kufahamu idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo. 
  Ikiwa na watu saba akiwemo  Mkemia Mkuu   wa Serikali, itakuja na majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na   zilitumika kemikali gani kuvikausha.
  Pia, jopo hilo litabaini kama ipo sheria na   ni ipi  inavunjwa. Wataalamu hao wanalenga kubaini, pia kama upo uzembe   katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya   mazoezi.
  Katika sakata hilo, lililovuta hisia za watu   na kuzua mjadala mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo   madaktari wa IMTU, walikamatwa  na Polisi kwa mahojiano, wakituhumiwa   kuhusika  katika  utupaji viungo vya binadamu jalalani.
  Kwa mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye   vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya   binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji  eneo la Bunju jijini   Dar es Salaam.

 
