(Picha na Genofeva Matemu)
Na Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikali – WHVUM
Tafiti zilizofanywa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania zinaonyesha kuwa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi nchini yamepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2011/2012 ambapo asilimia 6.2 ni wanawake na asilimia 3.8 ni wanaume.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Dr. Jerome Kamwela jana katika Viwanja vya Sabasaba alipokutana na waandishi wa Habari katika banda la TACAIDS kuwaelezea hali halisi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi nchini.
Dr. Kamwela amesema kuwa TACAIDS imekua ikifanya ukaguzi wa tafiti (takwimu) zilizokusanywa katika maeneo mbalimbali nchini na kuzitathmini tafiti hizo kama zina viwango wakiwa na lengo la kupanga mikakati itakayowawezesha kuelekeza rasililmali ili kuondoa maambukizi mapya yanayoweza kujitokeza.
"Tafiti zinaonyesha kuwa Mkoa wa Njombe unaongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 14.7 ambapo Iringa ina asilimia 9.1 ya watu walioathirika na Virusi vya Ukimwi na Mbeya ikiwa na asilimia 9, kwa upande wa mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ni Manyara na Kilimanjara ikiwa na asilimia 2 ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi" amesema Dr. Kamwela.
Akizungumzia kuhusu changamoto ambazo TACAIDS imekua ikizipata katika ukusanyaji wa takwimu za watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini Dr. Kamwela amesema kuwa uhaba wa wataalamu, uhaba wa vyuo vinavyofundisha taaluma ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na uhaba wa fedha kwaajili ya kufuatilia na kutathimini hali halisi ya maambukizi ya Ukimwi nchini vimekua vikizuia malengo ya kutokomeza Ukimwi nchini.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano kutoka TACAIDS Bw. Godlease Malisa amesema kuwa TACAIDS imekuja na mkakati unaozingatia sifuri tatu (three zeros) ukiwa na maana sifuri ya kwanza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi yashuke hadi sifuri, huku sifuri ya pili ikimaanisha unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi upingwe hadi sifuri na sifuri ya tatu ikimaanisha maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yapunguzwe hadi sifuri.