Saturday, July 05, 2014

Rose Muhando kupeleka Pindo la Yesu Mwanza



Rose Muhando kupeleka Pindo la Yesu Mwanza

MWIMBAJI mahiri nchini, Rose Muhando anatarajia kutambulisha kwa mashabiki wake albamu ya Kamanda Pindo la Yesu Agosti 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Albamu hiyo itazinduliwa Agosti 3 mwaka huu ukumbi wa Diamond, Jubilee Dar es Salaam na baada ya hapo itatambulishwa katika mikoa kadhaa nchini.

Taarifa ya mwimbaji huyo kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa tayari mkoa wa Mwanza umekuwa chaguo lake la kwanza baada ya uzinduzi wa Dar es Salaam."Nitazindua Diamond Jubilee Agosti 3, baada ya hapo nitaenda Mwanza Agosti 10 Uwanja wa CCM Kirumba, naomba mashabiki wangu wajiandae kupata vitu vizuri sana."Nimejipanga kuhakikisha nawapa burudani ya nguvu, najua nini wanakitaka, pia najua waimbaji gani wanawapenda, nipo katika utaratibu wa kuhakikisha wanafurahi," alisema Muhando.

Kwa mujibu wa Muhando, nyimbo zilizopo katika albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu ni Bwana Niongoze, Wewe Waweza, Usiniache, Nibariki, Muongo, Kwema, Kamata Pindo la Yesu na Facebook.

Hivi sasa Muhando anatamba na albamu yake ya Utamu wa Yesu yenye nyimbo saba, ambazo ni Utamu wa Yesu, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia.

Mbali na Utamu wa Yesu, Rose Muhando pia amewahi kutamba na albamu za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawasawa, Kitimutimu, Mungu Anacheka, Wololo.Pia amepata kung'ara katika wimbo wa Vua Kiatu, alioshirikiana na Anastazia Mukabwa wa Kenya.