Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu wawili wanaoshukiwa kuwa majambazi ambao walikutwa wakiwa na bunduki mbili aina ya shortgun zikiwa zimekamatwa vitako huku moja ikiwa imefungiwa hirizi kama kinga ya kuzuia wasikamatwe katika matukio ya uhalifu.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro Bw Robert Boaz amesema, watu hao Ibrahimu Machaku na Laurenti Massawe wamekamatwa juzi na jana katika oparesheni maalum ya kupambana na matukio ya uhalifu ambapo pia walifanikiwa kukamata kilo 4.5 za dawa za kulevya aina ya Cocain kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.
Kamanda Boaz amewaambia waandishi wa habari kuwa Massawe ambaye ni mkazi wa Arusha pia alikamatwa akiwa na vitu vya dhahabu na simu mbili ambavyo aliporwa mfanyabiashara mmoja mjini Moshi Bw Mehboob Sadiki baada ya kuvunjwa nyumba yake Juni 22.
Amesema, katika oparesheni hiyo polisi walikamata dawa hizo zikiwa zimetelekezwa na abiria aliyekuwa akisafiri na ndege kutoka Brazil kupitia Ethiopia, Mombasa hadi kwenye uwanja huo na jeshi la polisi limeanza kumsaka abiria huyo ambaye alitoweka.