Wananchi wanaoishi kando                ya maeneo ya ardhioevu na sehemu ambazo mito inakutana na                bahari wamehimizwa kuzingatia matumizi bora ya maeneo hayo                ili yasiweze kuleta madhara ya mali, uhai wao na uharibifu                wa viumbe hai vilivyopo katika sehemu hizo. 
        Naibu Waziri, Wizara ya                Maliasili na Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa, alisema hayo                wakati akifunga mkutano wa wanasayansi toka Afrika na nje                ya bara hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.                Kongamano hilo lililojulikana kama Afrideltas liliangalia                na kuchambua mabadiliko yanayotokea sasa katika maeneo ya                ardhi oevu na makutano ya mito na bahari. 
        Waziri Mgimwa alisema                serikali imeyachukua mapendekezo ya wanasayansi hao kwa                kuwa yanalenga kulinda maeneo hayo yaweze kutumika kwa kwa                faida ya sasa na vizazi vijavyo. 
        Pia alisema kuwa                serikali itahakikisha sera, sheria na kanuni mbalimbali                zinafuata maelekezo ya kitalaamu kama yaliyotolewa katika                kongamano hilo kwa vile maeneo hayo yanafaida kubwa za                kiuchumi. 
        "Katika kuhakikisha                jambo hili linafanikiwa, wadau wote wanatakiwa kushiriki                katika kutoa elimu ya mazingira kwa wakazi wa maeneo                hayo,"alisema. 
        Alisema Tanzania ina                changamoto ya kulinda aina mbalimbali za viumbe katika                maeneo ya ardhioevu ambavyo vipo katika hatari ya kutoweka                kutokana na shughuli za kibinadamu. 
        Naye, mjumbe wa kamati                ya maandalizi ya Kongamano hilo, Prof. Amos Majule ambaye                pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA)                ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kongamano                hilo lilikuwa na faida kubwa kwa washiriki hao wa                kimataifa.
        "Kila mmoja alijifunza                toka kwa mwenzake na kubadilishana uzoefu na kutoa                mapendekezo tuliyoona yanafaa," alisema. 
        Alisema moja ya                mapendekezo hayo ni kuona elimu mbadala inatolewa zaidi                kwa jamii jinsi ya kutumia na kulinda rasilimali zilizopo                katika maeneo ya ardhioevu na maeneo mito inapokutana na                bahari. Pia alisema watunga sera na watoa maamuzi                wameshauriwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili rasilimali                zinazopatikana katika maeneo hayo ziweze kutumika kwa                faida ya sasa na vizazi vijavyo. 
        Alisema changamoto                iliyojitokeza ni kwamba kuna njia zisizo endelevu za                matumizi ya madawa ya mbolea katika Kilimo, ukataji misitu                na ujenzi wa makazi katika maeneo hayo na kuleta athari za                kimazingira. Aliongeza kusema kuwa kutokana na mabadiliko                ya tabia nchi, maeneo hayo pia yanakumbwa na mafuriko na                kuathiri mazao ya Kilimo, uvuvi na makazi yao jambo ambalo                ni hatari kwa uhai wao. 
        Naye Mradibu wa Kenya                Wetlands Biodiversity, Dk. Wanja Njingi alisema kutokana                na tafiti zilizowasilishwa katika mkutano huo, nchi za                Africa zimefaidika na mawazo na taarifa mpya ya jinsi ya                kushughulikia na kulinda maeneo ya ardhioevu.
         "Kupitia tafiti hizi                sasa tunaweza kurekebisha mambo yaliyoharibika katika nchi                zetu," aliongeza kusema. 
        Kongamano hilo                lilijumuisha wanasayansi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo                Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Sudan, Senegal, Nigeria,                Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji na mwenyeji Tanzania. Pia                wanasayansi hao walitembelea Bonde la Mto Rufiji kujionea                hali ya bonde hilo na shughuli zinazoendelea. 
                 Naibu Waziri, Maliasili na                  Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa (katikati)akiongea wakati wa                  kufunga kongamano la kimataiafa la wanasayansi                  lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine katika picha ni,                  Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini Raslimali (IRA) ya                  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Amos Majule                  (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara                  hiyo, Dkt. Iddi Mfunda.
        Naibu Waziri, Maliasili na                  Utalii, Bw. Mahmoud Mgimwa (katikati) akifurahia jambo                  wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la wanasayansi                  lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine                katika picha ni, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini                Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),                Prof. Amos Majule (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi wa                Sera na Mipango wa wizara hiyo, Dkt. Iddi Mfunda (kushoto)                na Dk. Catherina Masao wa IRA (kulia) .
        

 
