Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na kubaini kuanza kwa uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba zinatokana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema: "Tuna makubaliano na Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji wa fedha, hivyo tuko katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano ya moja kwa moja kwa sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa katika utoaji wa taarifa."
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.
"Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini kutokana na uwezo wao mdogo tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema tunazo kesi tano hivi… ni kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu masuala ya fedha. Hatuwezi kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa na mkataba wetu na taasisi tunazofanya nazo kazi."
Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema wanaochunguzwa katika kesi hizo wanahusishwa na kampuni hewa zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha kisha kwenda kuzificha nje ya nchi.
"Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa wakipokea rushwa au wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni kivuli na ushirika mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda kwenye kampuni fulani kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na wafanyabiashara kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha," alisema.
Jaji Werema
Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini akakataa katakata kutaja watu wala kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.
"Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili, tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.
"Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu kwa utaratibu ili tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani tumekaa kimya hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika mtaona na mtasikia."