Friday, June 27, 2014

HATARI SANA...MARCIO MAXIMO NDIO HABARI YA MJINI...STORI KAMILI IKO HAPA...!



HATARI SANA...MARCIO MAXIMO NDIO HABARI YA MJINI...STORI KAMILI IKO HAPA...!

Kocha Marcio Maximo.
Hans Mloli na Wilbert Molandi
WAKATI Gazeti la Championi linaanza kuripoti juu ya ujio wa Kocha Marcio Maximo mnamo Mei 24, ambapo pia ndiyo lilikuwa gazeti la kwanza kabisa kuripoti juu ya Mbrazili huyo kuja nchini kuinoa Yanga, ilionekana kama ni ndoto, hatimaye neno limetimia.


Maximo, kocha wa zamani wa Taifa Stars, amerejea nchini jana, maalum kwa kazi moja tu, kuinoa Yanga, tukio ambalo limepokewa kwa shangwe na mamilioni ya mashabiki na wadau wa Klabu ya Yanga.

Mashabiki wa timu ya Yanga.
 Maximo hakuipa Yanga siku nne
Kutokana na awali kutolewa kwa taarifa za kutatanisha juu ya ujio wa kocha huyo, huku ikielezwa kuwa Mbrazili huyo angewasili Jumanne au Jumatano (siyo Championi lililoripoti hiyo habari), Championi Jumatano likaweka wazi kuwa Maximo angewasili mchana wa Alhamisi (Juni 26), ambavyo ndivyo ilivyokuwa, mamia ya mashabiki walijitokeza kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kumpokea.

Furaha ya mashabiki hao iliongezeka maradufu baada ya kuona sura ya Mbrazili huyo ikijitokeza na kujikuta wakipiga kelele huku wakishangilia kwa nguvu.

Maximo ambaye amesaini mkataba wa kuifundisha Yanga kwa miaka miwili, aliwasili saa 7.55 mchana akiwa pamoja na msaidizi wake ambaye pia ni Mbrazili, Leornado Leiva Martins na kupokewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu aliyekuwa ameambatana na Ofisa Habari, Baraka Kizuguto.
Akiongozwa na walinzi kadhaa na askari polisi.
Ulinzi mkali
Kutokana na umati mkubwa wa mashabiki, ilibidi kocha huyo apitishwe upande wa lango la kutokea la VIP la uwanjani hapo huku akiongozwa na walinzi kadhaa na askari polisi, ambako huko nako mashabiki waliruka uzio na kwenda kumsubiri kuona akijitokeza.
Maximo azungumza
Baada ya kutua, Maximo alizungumza machache ambapo aliwashukuru wapenzi na mashabiki wa Yanga na Tanzania kwa jumla kwa kwenda kumpokea huku akisisitiza kuwa anasikia faraja kurejea Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi tena.

"Nashukuru kurudi Tanzania, ni marafiki zangu na ninawapenda wote, nawashukuru pia waliokuja kunipokea, sina mengi nafikiri yote tutazungumza kesho (leo) kuhusu mipango na mikakati mizima ya timu na ujio wangu Yanga," alisema Maximo.

Baada ya hapo msafara kuelekea klabuni, Jangwani, Kariakoo ulianza huku ukisindikizwa na mashabiki kwa nderemo na vifijo.
Askari amvaa Maximo
Wakati msafara ukiwa barabarani kuelekea Jangwani, askari mmoja wa usalama barabarani alishindwa kuvumilia na kutaka kuvuka barabara ili akampe mkono Maximo, lakini ilishindikana baada ya foleni kuruhusiwa na askari huyo ambaye alikuwa ameanza kupiga hatua kurudi nyuma mikono mitupu.
 Mashabiki wabeza ujio wa Maximo
Wakati msafara ukiwa njiani, mashabiki wengi wa Simba, waliokuwa makao makuu ya klabu yao Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo ambapo msafara wa kocha huyo ulipita, walisikika wakibeza ujio wa kocha huyo na kuanza malumbano ya hapa na pale na wale wa Yanga waliokuwa kwenye msafara.
Maximo atua Jangwani
 Kocha huyo alipotua klabuni alilakiwa kwa shangwe kubwa na mashabiki, kisha kusaini kitabu cha wageni na baada ya muda akazungushwa kwenye Jengo la Yanga, baadaye akaenda kuwasalimia wazee wa klabu hiyo.

Safari kwa Manji
Mara baada ya kumaliza kilichompeleka Jangwani, Maximo alianza safari kuelekea Quality Plaza ambapo ndipo ilipo ofisi ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.

Aidha, taarifa zilizozifikia Championi Ijumaa ni kuwa, kiungo mshambuliaji Andrey Coutinho raia wa Brazil aliyetakiwa kuongozana na Maximo, anatarajiwa kutua siku yoyote kuanzia leo Ijumaa.