Afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Mbeya, Benard Winga ambaye ndiye mwezeshaji wa semina akiendelea kutoa somo.
Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Mbeya Rehema Matingisa akiendelea kutoa somo kwa washiriki wa semina.
Mratibu Ukimwi Wilaya ya Mbeya, Kelvin Kisoma akisisitiza jambo kwa washiriki wa Semina hiyo.
Wawezeshaji wakiangalia jambo kwenye kompyuta yao ikiwa ni kuweka sawa mikakati kabla ya kuanza semina.
2.
Washiriki wa semina wakifuatilia kwa makini kutoka kwa wawezeshaji semina kuhusu Ukimwi Wilaya ya Mbeya.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya mkoani hapa inaendesha semina ya siku mbili kwa wadau wa kudhibiti Ukimwi wilayani humo ili kufikia malengo ya Sifuri tatu.
Semina hiyo inafanyika Juni 18 na 19, Mwaka huu katika ukumbi wa kituo cha Walimu kilichopo Mbalizi Wilaya ya Mbeya mkoani hapa.
Semina hiyo imehudhuriwa na wadau ambao ni sekta binafsi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, viongozi wa dini, Wazee, Vijana na asasi binafsi kutoka wilayani hapa.
Akizungumza kwenye semina hiyo,Mratibu wa Ukimwi Wilaya ya Mbeya, Kelvin Kisoma, amesema mpango mkakati wa mwaka uliopita wa 2007/2008 ulioishia 2011/2012 umeonesha mafanikio makubwa kutokana na kupungua kwa maambukizi mapya ya Virusi vya ukimwi kwa asilimia 4 jambo linaloonesha mafanikio kuelekea sifuri tatu.
Amesema katika kipindi hicho kulikuwa na maambukizi ya asilimia 13 lakini baada ya kuanza utekelezaji wa mpango huo wa sifuri tatu imefikia asilimia 9 ambazo ni malengo yao kuwa zitapungua katika mpango wa miaka mitano ijayo.
Kwa upande wake mmoja wa wawezeshaji wa Semina hiyo ambaye pia ni Mratibu Msaidizi wa Ukimwi Wilaya ya Mbeya, Edah Misana, ameongeza kuwa katika mpango mkakati wa miaka mitano ijayo Halmashauri imejiwekea mikakati mbali mbali ili kuhakikisha wanafikia malengo ya sifuri tatu ambazo ni kuhakikisha kuwa hakuna maambukizi mapya, kupunguza unyanyapaa pamoja na vifo vinavyotokana na Ukimwi.
Ameitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kulenga makundi ambayo ni vijana walioko mashuleni na wasio mashuleni, walemavu, walioko kwenye ndoa, viongozi wa dini, wazee na watu mashuhuri.
Amesema kwa kuanzia hivi sasa Halmashauri imefanikiwa kuanzisha klabu kumi za kudhibiti ukimwi mashuleni kutoka kwenye kata Kumi ndani ya Halmashauri hizo.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Semina hiyo, Benard Winga ambaye pia ni Afisa Maendeleo Wilaya ya Mbeya, amesema mafanikio ya kufikia sifuri tatu yatafanikiwa endapo jamii itakubali kubadilika na kuitikia na kuungana na Halmashauri katika kupambana na maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Ameongeza kuwa Halmashauri inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ambapo alizitaja baadhi kuwa ni pamoja na baadhi ya waathirika kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi(ARV).
Amezitaja changamoto zingine kuwa ni pamoja na mgongano wa kiimani juu ya matumizi sahihi ya kinga zikiwemo Kondomu kuwa baadhi ya dini imani zao zinapinga pamoja na wataalamu wa tiba asili kutoa tiba za ukimwi bila kuzingatia vipimo sahihi.
Na Mbeya Yetu