Friday, June 20, 2014

BARAZA LA WAZEE KANISA LA MORAVIAN TABATA LAWATOA HOFU WAUMINI, LAKANUSHA TAARIFA YA KUZUILIWA KWA IBADA


BARAZA LA WAZEE KANISA LA MORAVIAN TABATA LAWATOA HOFU WAUMINI, LAKANUSHA TAARIFA YA KUZUILIWA KWA IBADA
Wakili wa kujitegemea wa Baraza la wazee wa kanisa la Moravian Usharika wa Tabata Bw. Benjamin Mwakambe akiongea na waandishi wa habari kuhusu amri ya iliyotolewa na mahakama kuzuia Bodi ya wadhamini wa kanisa la Moravian Kanda ya Kusini kusimamisha huduma za kiroho na kijamii katika eneo hilo. Wengine ni Mzee Kiongozi wa Usharika huo Bw.Ernest Isakwisa(kulia) na Hamphrey Mgema (kushoto)
Baadhi ya Wazee wa Kanisa la Moravian usharika wa Tabata wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari. Picha na Aron Msigwa -MAELEZO.

Uongozi wa Baraza la wazee wa Kanisa la Moravian usharika wa Tabata jijini Dar es salaam umekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa huduma za kiroho na kijamii katika ushirika huo zimesimamishwa kufuatia mgogoro wa uongozi wa usharika huo kupelekwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kwa niaba ya Baraza la wazee wa usharika wa Moravian Tabata Mzee Kiongozi, Bw. Humphrey  Mgema amesema kuwa  usharika huo ambao uko chini ya jimbo la Mashariki linaloongozwa na Mwenyekiti,Mchungaji Dkt.Clement Fumbo umekuwa katika mgogoro wa uongozi kwa zaidi ya miaka 2 na uongozi wa jimbo la Kusini linaloongozwa  na Askofu Lusekelo Mwakafwela.

 Amesema tofauti za uongozi na hasa baraza la wazee wa usharika huo  kutokubaliana na baadhi ya maagizo ya askofu Mwakafwela na Bodi ya Wadhamini kuhusu umiliki na uangalizi wa usharika huo vimesababisha Bodi hiyo kwenda mahakamani kuzuia kufanyika kwa shughuli zozote katika eneo la usharika huo. 

"Yapo mambo mengi ambayo ni kiini cha mgogoro huu lakini jambo kubwa ni hatua tuliyoichukua ya kutokubaliana na baadhi ya maagizo yake ambayo yalionekana kutolinufaisha kanisa na hasa madai ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Moravian kanda ya kusini kututaka sisi tutamke wazi kuwa wao ndio wamiliki halali wa kanisa hilo" Amesema.

Ameeleza kuwa tamko la maaskofu lililotolewa na mwangalizi wa Kanisa la Moravian jimbo la Kusini askofu Lusekelo Mwakafwela katika ushirika wa Kinondoni kuzuia ibada na shughuli za kijamii katika usharika wa kanisa hilo eneo la Tabata halikubaliki na kuongeza kuwa limeleta athari kwa washirika wa kanisa hilo zaidi ya 700 na kuwafanya baadhi yao kushindwa kuhudhuria ibada.

Aidha,amesema  kufuatia mgogoro huo kushindwa kupatiwa ufumbuzi katika ngazi za juu za kanisa hilo na hatua iliyochukuliwa ya kuwapeleka mahakamani wao kama baraza la wazee wameamua kuadai haki yao kupitia Wakili wa kujitegemea Bw. Benjamin Mwakambe.

 Amesema kuwa licha ya baadhi ya mashauri kuendelea kusikilizwa mara mahakama imetoa Amri kuwa shughuli za ibada na kijamii katika usharika huo ziendelee kama kawaida.

Kwa upande wake wakili wa kujitegemea wa Baraza la wazee wa kanisa hilo Bw. Benjamin Mwakambe amefafanua kuwa hukumu ya mahakama iko wazi na kuongeza kuwa maombi ya Bodi ya wadhamini yalikataliwa mahakamani.

"Mahakama imeshaamua katika masuala haya kuwa ile jamii iachwe na wala isibugudhiwe na mtu yeyote na kama kuna usumbufu wa aina yoyote utakaofanywa dhidi yao ni wazi watakuwa wamedharau amri ya mahakama"