Monday, May 12, 2014

TANZANIA YASISITIZA UWEZESHWAJI WA NCHI MASKINI

 
 
 

Balozi Tuvako Manongi,  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  akijiandaa kuwasilisha mchango na maoni ya Tanzania  wakati wa  Mkutano wa kumi na Moja wa Kikundi  Kazi cha Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa. Kikundi  Kazi hicho ambacho Tanzania ni  mjumbe kilikutana wa wiki moja  ambapo kilipitia na kuboresha rasimu ya malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015. Walio  kaa nyuma wa Balozi ni  Dr. Lorah Madete, Afisa Mkuu kutoka  Ofisi ya Rais-Tume ya  Mipango na Bw. Noel Kangada Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu
Dr. Lorah Madete akimpongeza mmoja wa Mwenyekiti- Mwenza  wa Kikundi   Kazi Mwakilishi wa Hungary Balozi Csaba Korosi mwishoni wa  mkutano wa 11 wa kikundi kazi hicho.  Pembeni anaonekana Mwakilishi wa Kenya, Balozi Macharia  Kamau ambaye  pia ni Mwenye Kiti- Mwenza wa kikundi hicho

TANZANIA YASISITIZA UWEZESHWAJI WA NCHI MASKINI
Na Mwandishi Maalum
Kikundi kazi cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichopewa jukumu la kupendekeza Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu baada ya 2015 ( SDGs) kimemaliza mkutano wake wa kumi na moja kwa kupitisha maazimio mbalimbali.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 30 zinazounda kikundikazi hicho na imeendelea kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba, matakwa ya nchi maskini na zinazoendelea yanazingatiwa ipasavyo katika maandalizi ya malengo hayo mapya ambayo yatachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs).

Wajumbe wa Kikundi kazi hicho walikutana kwa wiki moja hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  na kazi kubwa iliyofanyika katika wiki hiyo moja, ilikuwa ni kupitia na kuboresha rasimu ya malengo mapya ya maendeleo iliyokuwa imeandaliwa na Wawakilishi wa Kudumu wa Kenya na Hungary ambao ni Wenyeviti -Wenza wa Kikundi Kazi hicho.

Rasimu hiyo ilijumuisha maeneo muhimu yaliyomo kwenye Malengo ya Millenia na ambayo yanahitaji msisitizo na msukumo zaidi katika mpango mpya wa maendeleo baada ya 2015. Maeneo hayo ni pamoja na kuondoa umaskni, kuhakikisha upatikanaji wa chakula, afya, elimu na uwezeshaji wa wanawake.

Aidha maeneo mapya yanayojumuishwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama,  nishati, miundombinu, utunzaji wa mazingira yakiwamo ya baharini, kuhakikisha usawa miongoni na baina ya nchi, na ujenzi wa jamii zenye amani, zinazo tingatia utawala bora na utawala wa sheria

Akichangia majadiliano ya uboreshaji wa rasimi hiyo,  Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katikaUmoja wa Mataifa, na ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa uwezeshaji makini wa nchi maskini na zinazoendelea.

Balozi Manongi alieleza kuwa nchi maskini na zinazoendelea zinapashwa kuwezeshwa ili kupitia uwezeshwaji huo basi ziweze kuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza malengo mapya ya maendeleo kama ilivyokubalika katika Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu uliofanyika  Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2012.

Aliyataja maeneo ambayo nchi maskini na zinazoendelea zinahitaji uwezeshwaji makini kuwa ni pamoja na , masuala ya biashara ambapo nchi zilizoendelea zinatakiwa kupunguza vikwazo vinavyozinyima nchi zinazoendelea kufaidi fursa za biashara ya kimataifa.

Vile vile Tanzania  imezitaka nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi maskini kujenga uwezo wa kuendesha sekta muhimu kama vile kilimo, uchukuzi, viwanda, elimu na afya, sekta ambazo Tanzania  inaamini ni muhimu kwa maendeleo.


Katika mkutano huo wa kumi na moja na ambao pia Asasi zisizo za Kiserikali zilipata pia fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao. Tanzania pia imezitaka nchi zilizoendelea na zinazoibukia kiuchumi kuzipatia nchi maskini teknolojia salama na uelewa utakazo ziwezesha kuongeza kasi ya maendeleo nchi zao.

Balozi Manongi akiwasilisha maoni ya Tanzania, pia alisisitiza suala  la upatikanaji wa fedha za ndani mathlani kupitia ukusanyajiwa mapato.

Pamoja na misaada na uwekezaji kutoka nje katika kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo.

Kikundi kazi kinatarajiwa kuhitimisha shughuli zake Julai 2014 kwa kuwasilisha taarifa yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye naye ataiwasilisha taarifa hiyo kwenye Kikao cha 69 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba  2014.

Taarifa hiyo pamoja na taarifa za michakato mingine kuhusu agenda ya maendeleo baada ya  2015, itakuwa ndio msingi wa majadiliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa yatakayohitimishwa mwezi Septembea 2015 katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambapo wanatataraji wa kupitsha agenda hiyo na malengo yamaendeleo endelevu ambayo ndiyo mrithi wa Malengo ya sasa ya Millenia.