Monday, May 19, 2014

MGEJA AMTAKA DR SLAA KUACHA SIASA ZA KITOTO KWA KUMSAKAMA KATIBU MKUU WA CCM TAIFA

 
 
 


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja amemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dr, Wilbroad Slaa kuacha siasa za kitoto kwa kumsakama Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kuacha kufanya vikao na Watumishi wa Umma na kuangalia miradi ya maendeleo pamoja na kuizindua.


Mgeja aliyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake mkoani Shinyanga  kujibu kauli ya Katibu  wa CHADEMA  aliyonukuliwa alipokuwa akisema katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanywa na UKAWA katika maeneo mbalimbali hapa nchini hususani katika Mikoa ya Arusha Iringa na Manyara.

Dr, Slaa alinukuliwa  akisema kuwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana Mkoani Tabora alikutana Walimu huku akijua kuwa hakupaswa kufanya kitendo hicho kwani kinyume cha sheria na pia alizindua miradi mbalimbali ya Serikali.

Dr, Slaa aliendelea kuhoji kuwa Katibu Mkuu huyo wa CCM amepata wapi mamlaka ya kuzindua miradi ya Maendeleo iliyochangiwa na Wananchi huku akijua CCM haijachangia kitu chochote ila ni Serikali ndiyo iliyotekeleza miradi hiyo.

Dr Slaa alisema kuwa kitendo hicho anachokifanya Katibu Mkuu huyo wa CCM na viongozi wenzake wa Chama hicho kushiriki katika kuzindua miradi ya maendeleo, atatangaza kama ni janga la kitaifa.

"Kitendo kinachofanywa na Katibu Mkuu wa CCM cha kushiriki katika kuzindua miradi ya Maendeo sisi tutatangaza kama ni janga la kitaifa na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuzuia kwa muda wa siku tatu la sivyo na sisi tutaanza kukutana na Watumishi wa Umma", Alinukuliwa Dr, Wilbroad Slaa.

Kufuatia hali hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja alisema kuwa Dr, Wilbroad Slaa anamuonea wivu katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kwa kazi nzuri na mafanikio ya kimaendeleo ya kukagua Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotekelewa na  Serikali yake.

Alisema kuwa Dr, Slaa na Wenzake watambue kuwa Chama cha Mapinduzi ndicho kilichofunga mkataba na Wananchi katika kipindi cha uchaguzi cha mwaka 2010/2015 kwa kupewa ridhaa ya kuongoza, kusimamia na kuleta maendeleo kupitia Serikali na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa muda huo cha kipindi cha miaka mitano.

Pia alimtaka kiongozi huyo na wapinzani wenzake kutambua kuwa hata mtoto mdogo wa darasa la pili anatambua nini maana uchaguzi na kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na kuongeza kuwa analolifanya Katibu Mkuu wa CCM na viongozi wenzake wa CCM kuwa wapo sahihi kwa mujibu wa dhamana waliokabdhiwa na Wananchi.

"Chama cha Mapinduzi kuisimamia Serikali yake sio dhambi kwani sawa na Mwenye shamba kukagua eneo lake na Mfugaji kukagua mifugo yake na tajiri wa mabasi kukagua mabasi yake kama yanafanya kazi na kuhudumia vizuri wateja wake",

"Nawashangaa Wapinzani kwa kauli zao za kujichanganya mbona Serikali ikifanya vibaya wanakuwa wa kwanza kulaumu na kusema Serikali ya CCM haijawatendea haki watanzania lakini ikifanya vizuri kama hivi sasa inapowaletea maendeleo wanachi wanakataa kuwa sio Serikali ya CCM", Aliongeza Mgeja.

Mgeja alifananisha lawama za kumlaumu Katibu Mkuu Kinana na Chama kwa ujumla kutimiza majukumu yake ya kuisimamamia Serikali yake  iliyokabidhiwa ridhaa na Wanachi kuiongoza ni kama kelele za chura ama mtu mzima kumtishia Nyau na kamwe katibu Mkuu hataacha kufanya kazi yake na kutimiza majukumu ya chama kuisimamia Serikali.