Thursday, October 04, 2012

WIZARA YAWATAKA WATUMISHI WA WANYAMAPORI KUIMARISHA UHIFADHI



Twiga akiwa katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha Iringa
Wanahabari Daud Mwangosi na Mahija Zayumba wakipiga picha ya pamoja na mmiliki wa mtandao huu Bw Francis Godwin( kushoto) katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha
 
Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Khamis Suedi Kagasheki amewataka askari wa Wanyamapori popote waliko nchini kufanya kazi kwa bidii na bila uoga wakati wanapotekeleza kazi zao za kila siku maana mafanikio ya uhifadhi hapa nchini yako mikononi mwao.
Aliwaasa watumishi wote wa Idara ya Wanyamapori kuzingatia ushirikiano (team work) ili kufanikisha uhifadhi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Alisema ushirikiano huo unawahusu watumishi wote wa Wanyamapori popote waliko nchini, yaani wale walioko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, TANAPA, Ngorongoro na Serikli za Mitaa.
Mheshimiwa Kagasheki aliyasema hayo jana katika kikao alichokiitisha cha viongozi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Makao Makuu ya Wizara pamoja na mameneja wa mapori yote ya akiba kilichofanyika Matambwe, kituo kilichoko katika Pori la Akiba la Selous. Alisema aliitisha kikao hicho ili kupata maoni kutoka kwa washiriki hao kuhusu namna ya kuboresha uhifadhi.
Kikao hicho cha siku mbili kilihudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Bw. Paul Sarakikya, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Bw. Alan Kijazi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) Dakt. Mduma. Wengine waliohudhuria ni Makamanda wa Kanda 8 wa Kikosi Dhidi Ujangili.
Washiriki wa kikao hicho walimshukuru Waziri kwa kutambua kazi yao na kuwatia moyo na wakaahidi kuwa wataendeleza mapambano wanayoendelea nayo sasa kwa bidii zaidi hususan ya kutokomeza ujangili.
Walimwambia Waziri kuwa ushindi wa vita dhidi ya ujangili utafikiwa maana wameshabadili mbinu za mapambano baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa majangili nao wanatumia mbinu na silaha za kisasa.
Waziri Kagasheki aliwaambia wahifadhi hao kuwa Wizara inao mkakati wa kuongeza fedha, raslimaliwatu na vitendea kazi kwa mapori yote nchini. Vitendea kazi hivyo ni kama vile magari silaha, na vifaa vya mawasiliano.
Alisema kuwa mafunzo kwa askari wa wanyamapori walioajiriwa hivi karibuni yanayoendelea Matambwe hivi sasa ni sehemu ya mkakati huo. Akiwa huko Waziri alipata fursa ya kukagua askari hao wapya wakiwa mafunzoni.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
4 Oktoba 2012