WAKULIMA wa zao la Cocoa wilayani Kyela mkoani Mbeya wametakiwa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya jamii ili wanufaike na dola 60,000 za Marekani sawa na Sh; M,110 zilizotolewa na Kampuni ya Bioland International Limited kwa ajili ya kuchangia sehemu ya gharama za bima hiyo kwa wakulima.
Meneja wa Biolands tawi la Kyela, Erasto Kilongo, alitoa wito huo wakati akikabidhi msaada wa vitabu vya kiada kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Kikuba wilayani Kyela vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 9.
Alisema kuwa fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya kuwawekea bima ya afya wakulima zaidi ya 15,000 wanaoiuzia kampuni hiyo cocoa, lakini waliojitokeza kujiandisha kwenye bima ya afya ni 6000 tu.
Alisema mkulima anayejiunga na bima ya afya anatakiwa kutoa shilingi 2000 na kampuni hiyo inamchangia shilingi 3000 ili kukamilisha kiasi cha shilingi 5000 ambazo zinahitajika kwa mwananchi kujiunga na bima ya afya na kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kampuni yake imejikita kutoa huduma za kijamii katika Nyanja tatu za afya, elimu na utunzaji wa mazingira na kuwa katika sekta ya elimu imeamua kusaidia upatikanaji wa vitabu katika shule za msingi ili kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu.
Kampuni hiyo ilitoa msaada wa vitabu katika shule sita, tatu zikiwa wilayani Kyela na nyingine tatu za wilayani Rungwe.
Vitabu vilivyotolewa ni vya masomo ya Hisabati, Jiogarafia, Kingereza, Sayansi na vitabu vya mwongozo wa mwalimu kwa masomo hayo kwa madarasa tofauti.
Shule zilizonufaika na msaada huo ni Ndubi, Matwebe, na Mbambo kwa wilaya ya Rungwe na shulle za wilayani Kyela ni Kikuba na Lubaga.