Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imetangaza kipindi cha pingamizi kwa waombaji uongozi katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ombeni Zavala, kipindi cha pingamizi ni kuanzia Oktoba 5 hadi 9 mwaka huu, na pingamizi ziwasilishwe ofisi za TWFA.
Mwisho wa kupokea pingamizi ni saa 10 kamili jioni, na hakuna ada kwa ajili ya pingamizi.
Pia amesema usaili kwa wagombea utafanyika kati ya Oktoba 12 na 14 mwaka huu kuanzia saa 3 asubuhi kwenye ofisi za TWFA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kila mgombea anatakiwa kufika kwenye usaili akiwa na vyeti vyake halisi (original) vya kitaaluma.
Waombaji wa uongozi kwenye uchaguzi huo ni Lina Paul Kessy, Isabellah Hussein Kapera na Joan Ndaambuyo Minja (Mwenyekiti) wakati mwombaji wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Roseleen Kissiwa.
Nafasi ya Katibu Mkuu imevutia wagombea wawili; Amina Ali Karuma na Cecilia Oreste Makafu. Mark Raghton Mhango ni mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa Rose Msamila anayewania nafasi ya Mhazini.
Wagombea wanne wameomba nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wagombea hao ni Furaha Emily Francis, Zena Suleiman Chande, Jasmin Badar Soud, Juliet Edwin Mndeme.
Wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Rahim Salum Maguza, Triphonia Ludovick Temba na Sophia James Charles.