KAMBI zinazosigana ndani ya CCM zinaonekana kuchuana vikali katika uchaguzi wa ngazi ya wilaya ya chama hicho tawala, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akionekana kupata mafanikio, ikilinganishwa na mahasimu wake, Benard Membe na Samuel Sitta.
Kama ilivyo kwa Lowassa, Sitta ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wamekuwa wakitajwa kuwa kwenye harakati za kuusaka urais, hivyo uchaguzi wa ndani wa CCM ni fursa ya kupanga safu za kufanikisha mikakati hiyo. Lowassa binafsi tayari amepita katika kinyang’anyiro hicho kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Wilaya ya Monduli.
Jana mbunge huyo wa Monduli alitoa kauli kali akisema kuwa wapo watu wanaovuruga CCM katika Wilaya ya Monduli na kwamba tayari amewabaini, hivyo kuahidi kwamba watashughulikiwa kisiasa. ''Yako maneno ya ovyoovyo yamekuwa yakipikwa ya kuwaandama viongozi wa CCM Monduli, yanasemwa na wakubwa fulani, yanapikwa na watu fulani wa Monduli, tunawajua. Nataka kuwaambia tumewajua na nawaambia hawatuwezi,'' alitamba Lowassa. Lowassa alisema ushindi alioupata umedhihirisha kuwa ana misuli ya kisiasa na kwamba wakazi wa Monduli ndiyo msuli huo.
''Kuna mzee rafiki yangu aliniambia kuwa katika kazi za siasa angalia ‘grassroots’. Watu wanakuwa ndiyo msuli wako kisiasa na mimi watu wa Monduli ndiyo msuli wangu,'' alisema. Aliendelea ''Wananchi wa Monduli mmenithibitishia hilo na nawashukuru sana kutoka kwenye ‘sakafu’ ya moyo wangu, jibu la thibitisho hilo kwangu ni utumishi uliotukuka.'' Kwa upande wake, Membe anasubiri kuparurana na vigogo wenzake katika kundi la kifo la ujumbe huo katika uchaguzi wa ngazi ya Taifa, wakati Sitta tayari ni mjumbe wa NEC akiwakilisha wabunge wa CCM katika chombo hicho kikubwa cha uamuzi ndani ya chama hicho. Matokeo katika maeneo kulikomalizika uchaguzi wa ngazi ya wilaya yanaonyesha kuwa Lowassa amefanikiwa kupanga safu yake vizuri zaidi, ikilinganishwa na wenzake hao.
Membe anaonekana kufuata kwa karibu na Sitta ni kama anashika mkia kwa kuwa na wafuasi wachache waliofanikiwa kuchaguliwa. Hata hivyo, chaguzi katika baadhi ya mikoa bado zinaendelea, huku uchaguzi wa ngazi za mikoa na taifa ukisubiriwa kwa hamu. Manyara na Arusha Kundi la Lowassa lilizidi kupata nguvu baada ya mfuasi wake mpya ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary Nagu kumbwaga Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye. Sumaye naye anatajwa kuwa miongoni mwa ‘wanaoutaka’ urais na kuanguka kwake katika uchaguzi wa Hanang, kunatia doa kubwa harakati zake hizo.
Katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye Wilaya ya Arusha Mjini, Lowassa ameibuka kidedea kwa wapambe wake kadhaa kuchaguliwa, huku mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Wilaya hiyo, Jubilate Kileo akiangushwa na Dk Wilfred Ole Soilel. Katika kinyang’anyiro cha mjumbe wa Nec, Godrey Mwalusamba alishinda na kuwaangusha vibaya wapinzani wake ambao ni Loota Laiser na Dk Harold Adamson.Kuchaguliwa kwa Dk Ole Soilel anayehusishwa na kambi la Lowassa kuliibua simanzi kwa kambi nyingine ambapo katika hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Katibu wa CCM Arusha, Mary Chatanda walionekana kuwa wanyonge muda wote.
Mwanza na Dodoma Mkoani Mwanza, kambi za Lowassa na Membe zinatajwa kuchuana vikali huku kukiwa na sintofahamu kwamba mgombea wa nafasi ya mweyekiti wa mkoa huo, Anthony Diallo yuko upande upi. Diallo ambaye alianguka katika uchaguzi wa ubunge Oktoba 2010, anaonekana kurejea kwa nguvu mpya, kwani tayari baadhi ya wale wanaotajwa kuwa wafuasi wake wametwaa nafasi muhimu katika uchaguzi wa wilaya.
Hata hivyo, kada huyo wa siku nyingi wa CCM ambaye anamaliza muda wake wa ujumbe wa NEC akiuwakilisha Mkoa wa Mwanza, anakabiliwa na kibarua kigumu Oktoba 13, mwaka huu, atakapopambana na mweyekiti anayetetea nafasi yake Clement Mabina, Zebedayo Athumani na Joseph Langula Yared. Kwa sasa kuna taarifa kwamba Diallo anamuunga mkono Membe hivyo ushindi wa wafuasi wake katika Wilaya za Nyamagana, Ukerewe, Misungwi na Sengerema unaweza kuinufaisha kambi hiyo.
Mabina ambaye anatajwa kuwa mshirika wa Lowassa, katika matokeo ya awali, kambi yake inaonekana kutokufanya vizuri. Ushindi muhimu katika Wilaya ya Nyamagana ulikuwa ni wa nafasi ya Mwenyekiti iliyonyakuliwa na msadizi wa siku nyingi wa Diallo, Raphael Shilatu, ambaye aliwabwaga Mashaka Kaguna aliyetajwa kuwa mfuasi wa Lowassa na Yahya Nyaonge anayetajwa kuwa mfuasi wa Sitta. Hata hivyo, ushindi huo unatajwa kutiwa doa na mmoja wa wafuasi wa Lowassa ambaye ni mbunge wa zamani wa Nyamagana, Lawrence Masha ambaye alikuwa mjumbe wa NEC.
Wilayani Ukerewe kambi ya Membe inatajwa kushinda kiti cha Uenyekiti kupitia Ally Mabile na katika Wilaya ya Busega kambi ya Sitta inatajwa kutwaa ujumbe wa NEC kupitia kwa mbunge wa zamani wa Busega, Dk Raphael Chegeni. Mkoani Dodoma matokeo ya uchaguzi wa nafasi mbalimbali yanaonyesha kwamba kambi ya Lowassa imefanya vizuri hasa katika Wilaya za Dodoma Mjini, Bahi, Kondoa, Chemba na Kongwa.
Hata hivyo, ngome ya Waziri Mkuu huyo wa zamani imeangukia pua katika Wilaya ya Chamwino, baada ya wapambe wake kubwagwa na wale wanaotajwa kumuunga mkono Sitta.
Katika Wilaya ya Mpwapwa viongozi waliochaguliwa ni wapya na hadi sasa haifahamiki wanaunga mkono kambi gani. Dar, Zanzibar na Moro Visiwani Zanzibar, Lowassa aliendelea kupeta kutokana na ushindi wa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Hamad Yussuf Masauni, ambaye alishinda nafasi ya ujumbe wa NEC na kumbwaga aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mahamoud Thabiti Kombo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Katibu wa Wilaya ya Mjini, Fatma Juma Shomari alisema kwamba kati ya wagombea 19 waliokuwa wakiwania nafasi sita za NEC, Masauni aliibuka mshindi wa pili akitanguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai. Aliyeshinda nafasi ya uenyekiti ni Juma Faki Chumu na wajumbe wengine wa NEC ni Buruhani Saadati Haji, Asha Abdalla Juma, Talib Ali Tali Sufiani Khamis Ramadhani na Omar Jastus Morris.
Hata hivyo, katika Mkoa wa Dar es Salaam, kambi ya Lowassa ilipata pigo kutokaana na kubwagwa kwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga aliyekuwa akiwania nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Ilala. Kadhalika mkoani Morogoro, kambi hiyo pia ilipata pigo kutokana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala kubwagwa na Suleiman Ahmed Sadiq katika uwakilishi wa NEC Wilaya ya Mvomero.
Taarifa kutoka mkoani Tabora zinasema katika wilya zote za mkoa huo, kambi ya Lowassa imeshinda kwa kishindo isipokuwa Wilaya ya Urambo ambayo kambi ya Sitta inadaiwa kuibuka kidedea. Wasomi wanena Baadhi ya wasomi nchini, wametofautiana kimtazamo kuhusu chaguzi ndani ya CCM huku wengine wakisema chama hicho kimeshindwa kuwadhibiti vigogo wanaotajwa kuwania nafasi ya urais ambao wamefanikiwa kuwaingiza wafuasi wao kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.
Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Sabun Parit alisema hatma ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ni nzuri kutokana na kufanikiwa kuendesha uchaguzi wake kwa utulivu. “Mara nyingi tumezoea kuona makundi yakiibuka wakati wa uchaguzi, lakini safari hii hali ni shwari, hatujasikia makundi wala malalamiko na hii ni ishara kwamba hiki chama kimekomaa na hakiwezi kutetereka,” alisema mhadhiri huyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitilya Mkumbo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema jana kuwa CCM imeshindwa kuwadhibiti vigogo hao ndani ya chama hicho na hivyo wameanza vizuri katika maandalizi ili kupitishwa na chama hicho kugombea kiti ya urais. “Kwa kweli CCM wamejimaliza na wameonekana kuwa hawana jipya, wale waliotaka kuwavua magamba ndiyo haohao wamepitishwa kwenye uchaguzi pamoja na wafuasi wao kuwasaidia katika Uchaguzi Mkuu,” alisema Dk Mkumbo.
Naye Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema CCM imeonyesha kwamba hakuna kiongozi yeyote mwenye hatimiliki ya chama hicho. “Kwa namna mambo yalivyoonyeshwa kwenye uchaguzi huo, mtu yeyote anaweza kuingia na kuondoka kwenye chama hicho,” alisema.
Naye Kisena Mabuba ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo cha Mwalimu Nyerere alisema uchaguzi huo umefuta makundi ndani ya CCM. “Tofauti na matarajio ya wengi kuwa CCM ingemeguka, mimi ninachokiona hapa kundi lililobaki na nguvu ni lile la mwenyekiti mwenyewe. Kundi moja limefutwa kabisa na mengine yameshindwa kupata nguvu za kutosha,” alisema Mabuba