Wednesday, October 03, 2012

TRL yaelezea mchakato wake wa kuanzisha usafiri wa treni jijini Dar



Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) unapenda kuwataarifu Wateja na Wananchi wa Dar es Salaamkwa ujumla kuwa taarifa iliyotolewa na Gazeti la kila siku la Mwananchi toleo la siku ya Jumanne Oktoba 02, 2012 kwambaSUMATRAndiyo kikwazo cha kuanza kwa huduma ya usafiri wa treni jijini Dar es Salaam siyo sahihi.

Katika mchakato wa kutoa  huduma za usafiri wa treni ambayo hapo awali haikuwepo jijini, wadau wa kufanikisha mradi huu  ni taasisi nyingi ambazo zinapaswa kuchangia kuanzishwa kwake.Hivyo basi mchakato huo ni wa lazima na hakuna njia ya mkato . Tunapenda kueleza wazi kuwa  siyo sahihi kusema kuwa TRL imekwama kuanza kutoa huduma ya usafiri wa treni ya  abiria jijini kutokana na SUMATRA kutoidhinisha viwango vya nauli na kutopewa leseni.

Uongozi wa TRL unapenda kutoa rai kwa Waandishi habari na Wahariri wao kabla ya kuchapishwa habari nyeti kama hii inayogusa maslahi ya Wadau wengi na hasa wale wanaongojea kwa hamu huduma hii ianze kujitosheleza  kuwa habari wanayoichapisha ni sahihi na kama inajenga au kubomoa.
  Ukweli ni kwamba TRL hivi sasa inakamilisha mchakato wa kuandaa na  kuwasilisha vigezo ambavyo vinahitajika na SUMATRA ili iweze kufanya tathmini yake na hatimaye kutoa leseni ya huduma ya treni jijini .

Tunarudia Uongozi wa TRL unasikitika kwa usumbufu uliotokana na taarifa hizo zisizo sahihi kwa Wadau wote na hasa kwa  Uongozi wa SUMATRA.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa
Niaba ya  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Mhandisi Kipallo A. Kisamfu
Dar es salaam,
Oktoba 2, 2012