Wednesday, October 03, 2012

CHADEMA ARUSHA YASHUTUMIWA KUTAFUNA RAMBIRAMBI ZA MJANE NA KUMTELEKEZA.


Mjane Asia Ismail ambaye ni mke wa marehemu Ismail Omary aliyeuwawa katika maandamano ya Chadema mnamo Januari 5 mwaka jana jijini Arusha, akiwa amembeba mtoto wake wa kike Amina Ismail katika mkutano wa hadhara wa Chama cha CUF uliofanyika uwanja wa Levolosi, ambapo amekishutumu Chadema kwamba kimetafuna fedha za rambirambi za marehemu mume wake na kisha kumtekeleza pamoja na kuahidi kumpatia. (Picha na Mahmoud Ahmad).

Mahmoud Ahmad – Arusha.

Mjane Asia Ismail ambaye ni mke wa Ismail Omary  aliyeuawa katika maandamano ya Januari 5 mwaka jana, amekishutumu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Arusha kwamba kimetafuna fedha za rambirambi za marehemu mume wake lakini mbali na hilo pia  wamemtelekeza.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Wananchi (Cuf) uliofanyika katika uwanja wa Levolosi, mjane  huyo amesema kwamba Chadema waliahidi kumpatia fedha za rambirambi zilizochangwa katika uwanja wa NMC wakati wa kuaga mwili wa mume wake lakini hadi leo hajazipata.

Huku akiangua kilio katika mkutano huo,  amesema kwamba alipewa taarifa  kwamba chama cha Chadema kinachangisha fedha za rambirambi na mara watakapokamilisha mchango hiyo watampatia, lakini  hadi leo hajawahi kuona fedha yoyote.

Mjane huyo aliyekuwa amembeba mtoto wake wa kike jukwaani aitwaye Amina Ismail  alitoa machungu hayo na  kwamba fedha aliyoambulia hadi sasa ni ile iliyotolewa na kada wa CCM Mustafa Sabodo kiasi cha shilingi milioni 5.

Hatahivyo, amesema kwamba mara kwa mara alikuwa akifunga safari kufika katika ofisi za  Chadema wilayani, kwa lengo la kufuatilia fedha za rambirambi za mumewe lakini badala yake alikuwa akipigwa danadana.