Thursday, September 27, 2012

WAZIRI MKUU WA ZAMANI UINGEREZA AIKUMBUKA TANZANIA



Waziri Mkuu wa Mstaafu wa Uingereza, Bw. Gordon Brown akizungumza wakati wa mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Afrika walipokuta Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa sambamba na majadiliano yanayoendelea ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa. Viongozi hao waafrika walikutana kujadiliana Azimio la mpango wa AU kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi ambapo pamoja na mambo mengine walikubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wake na uwekezaji ili kuukabili ugonjwa huo. Katika Mchango wake, Bw. Brown ambaye ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, aliwahimiza viongozi hao (hawapo pichani) kuhakikisha kwamba wanaipa elimu umuhimu wa pekee kwa sababu ni kwa kupitia elimu ndipo wananchi wanaweza siyo tu kujikinga na maambukizi bali hata kuudhibiti ugonjwa huo. Katika maelezo yake alielezea pia namna alivyotiwa matumaini na mtoto mdogo wa kitanzania alipoitembelea Tanzania mwaka 2005 na kupata fursa ya kumpakata mtoto huyo ambaye alifiwa na wazazi wake wote wawili, ili hali yeye mwenye akiwa ameambukizwa na akiugua kifua kikuu, lakini pamoja na udhaifu wote mtoto huyo alionyesha macho ya matumaini. Ni matumaini aliyoyaona kwa mtoto huyo ndiyo yanayomfanya mpaka leo hii , Gordon Brown kuamini kwamba yapo matumaini ya kuukabili ukimwi kupitia mipango mbalimbali na kubwa zaidi fursa ya kila mtu kupata Elimu.
Wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Rusibamayila na Dk. Mmbado wakifuatilia mkutano wa viongozi wa afrika kuhusu ukimwi.
Mhe. Vita Kawawa akifuatilia mkutano wa wabunge wanaohudhuria mkutano wa 67 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. mkutano huo uliandaliwa na  Inter-Parliamentary Union ( IPU), katika mkutano huo wabunge walibadilishana mawazo kuhusu wajibu wa  mabunge na wabunge katika kusimamia utawala wa sheria, kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa ya kuzijua sheria zilizopo pamoja na mbinu mbalimbali zilizolenga kuwajengea  uwezo wabunge wa kuzifahamu sheria na kuzijengea hoja.  Aidha wabunge hao  walielezwa kwamba mbunge anayechaguliwa kwa njia halali bila rushwa au sheria kupindishwa anakuwa na nafasi nzuri ya kusimamia sheria na kuzitetea n akuwatetea wananchi. Kwa upande wake Mbunge  Kawawa akichangia majadiliano hayo aligusia pamoja na mambo mengine mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu, nafasi ya bunge  katika kuisimamia serikali pamoja na uundwaji wa taasisi mbalimbali zinazolenga kumsaidia mwananchi wa kawaida kupata haki zake za kisheria.
Waziri wa Katiba na Masuala ya  Sheria kutoka Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar Mhe. Abubakar Khamis Bakari ( Mb)  akichangia majadiliano kuhusu  Ujenzi wa Amani: kuelekea amani endelevu na usalama. Mkutano huo wa Kilele ulikuwa umeandaliwana kamisheni ya Ujenzi wa Amani. katika mchango wake Waziri Khamis pamoja na mambo mengine alisema kwamba   Tanzania ikiwa nchi Mwanzilishi wa   Tume ya Ujenzi wa  Amani ya Umoja wa Mataifa ilikuwa inasisitiza  umuhimu wa nchi zinazotoka katika vita kumiliki yenyewe ajenda zake za maendeleo na ujenzi wa nchi zao badala ya kupandikiziwa ajenda au  nini wanatakiwa kufanya kwa vile tu wanahitaji kusaidiwa. aidha akasema  Tanzania inaamini zaidi katika vitendo badala ya maneno na ahadi zisizotekelezwa.
Ujumbe uliofuatana na  Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa uzinduzi wa  Taarifa ya   Kamisheni ya Kimataifa ya masuala ya  Uchaguzi, Demokrasia na Usalama hiyo, uzinduzi ambao umefanyika  sambamba na   Mkutano wa 67 wa  Baraza  Kuula Umoja wa Mataifa. RTaarifa hiyo inasisitiza umuhimu wa uadilifu katika chaguzi mbalimbali, ambapo nchi zote duniani isipokuwa 11 zimefanya chaguzi katika miaka ya hivi karibuni.  Kutoka kushoto ni Balozi Liberata Mulamula, Mhe. Vita Kawawa (Mb),   Katibu Mkuu Kiongozi na  Mhe. Musa Hassan Mussa (Mb).
 Katibu Mkuu  Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, akichangia majadiliano wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ilyoandaliwa na Kamisheni ya Kimataifa ya masuala ya Uchaguzi, Demokrasia na Usalama. kamisheni hiyo inaongozwa na  Bw. Kofi Anna, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa. katika mchango wake, katibu Mkuu Kiongozi  alisema misaada au ufadhili hasa kutoka nje unaleta changamto kubwa  hasa ikizingatiwa kwamba nchi  nyingi zinazoendelea hazina mifumo ya udhibiti wa misaada hiyo. aidha pia akasema nchi nyingi zinachangamoto ya kujenga utamaduni wa vyama vya  upinzani kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kutoa ushirikiano  kwa chama tawala   ili  kitekeleze ilani yake kwa mafanikio na kwa faida ya wananchi waliowachagua. kama hiyo haitoshi akaongeza kwamba Tanzania inaheshimu na kuthamini ushiriki na  mchango wa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makundi ya wanawake na  imedhamiria kufikia ushiriki wa asilimia hamsini kwa asilimia hamsini baina ya wabunge wanawake na wanaume.