Wednesday, September 12, 2012

Tendwa, Chadema Sasa Jino Kwa Jino



 

MVUTANO kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umechukua sura mpya baada ya chama hicho kutangaza uhasama dhidi yake kikieleza kuwa hakiko tayari kufanya naye kazi hadi atakapowaomba radhi.

Wakati Chadema kikisema hayo, Msajili huyo amejibu madai hayo akisema hatakubali kuona chama hicho kikikaidi maagizo yake, likiwamo la kusitisha Operesheni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

Septemba 4, mwaka huu Tendwa alitishia kukifuta Chadema baada ya matukio ya vurugu katika mikutano yake ukiwamo ule uliofanyika Iringa na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.

Baada ya kauli hiyo, chama hicho kilijibu mapigo na kumtaka msajili huyo aanze kwanza kukifuta Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Msimamo wa Chadema
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maazimio ya mkutano wa dharura wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kujadili hali ya siasa nchini, uliofanyika Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uadui na Tendwa akisema chama hicho hakitafanya kazi na Ofisi ya Msajili mpaka Tendwa atakapoondolewa.

Mbowe alisema Chadema kimefikia uamuzi huo kwa madai kuwa msajili huyo anafanya kazi kwa kuegemea upande mmoja wa CCM.

“Kutokana na utendaji dhaifu wa Tendwa unaoegemea upande mmoja na uliojaa ‘propaganda’, Kamati Kuu ya Chadema imetangaza kuwa Tendwa ni adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyonayo,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Kamati kuu imeazimia kuendelea kuheshimu sheria ya vyama vya siasa, lakini Chadema haitashiriki shughuli yoyote itakayosimamiwa na Tendwa hadi atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa mtu mwingine.”

Mbowe alisema matamshi na barua zinazotolewa na msajili huyo dhidi ya Chadema zinaonyesha kuwa yupo katika nafasi hiyo kwa masilahi ya CCM hivyo akiendelea kushika wadhifa huo ataliingiza taifa katika vurugu.

Tendwa ajibu mapigo
Tendwa alisema hatakuwa tayari kuona Chadema kinaendelea kufanya maandamano ambayo alidai ndiyo chanzo cha kuibuka kwa vurugu nchini. Alisema Sheria ya Vyama vya Siasa ipo wazi na hatasita kuitumia kukiadhibu.

“Sheria zipo na taratibu za kufuata zipo, tutachukua hatua, hatuwezi kuona mikutano inafanyika na watu wanakufa halafu tuendelee kukaa kimya. Wao si wanapingana na mimi, ngoja tu sheria itachukua mkondo wake, hili si tatizo maana sheria zipo wazi kabisa.”

Alisema tayari alishatoa tahadhari kwa chama hicho lakini anaona bado kinaendelea kukaidi maagizo yake.
Katika kauli yake ya Septemba 4, mbali na kutishia kukifuta Chadema pia alisema atachukua uamuzi huo kwa chama chochote cha siasa ambacho kitakaidi amri za polisi na kusababisha vurugu.

Alisema mfululizo wa mauaji ya wananchi katika mikutano ya siasa unatokana na vyama hivyo kukinzana na polisi na wakati mwingine, kutumia lugha za matusi na vitisho vingine dhidi ya wabunge halali wa majimbo husika.

Wamshukia Nchimbi, Mwema
Katika hatua nyingine, Chadema kimewataka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, Mkuu wa Operesheni ya Jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile wajiuzulu nyadhifa zao.

Mbowe alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na watu kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi ambao wanasimamiwa na viongozi hao.

Mbowe alisema kuwa chama hicho hakiko tayari kufanya kazi na kamati ya kuchunguza tukio zima lililosababisha kifo cha Mwangosi, ambayo iliteuliwa na Dk Nchimbi.

Sambamba na hilo, chama hicho pia kimeitaka Serikali kuwakamata na kuwafungulia mashtaka ya mauaji Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Morogoro na askari waliohusika katika vurugu za Morogoro na Iringa ambazo zilisababisha vifo.

Mbowe alisema kukamatwa kwa maofisa hao kutawafanya viongozi na watawala wengine kufanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na kutambua na kuthamini uhai wa binadamu.

“Kutokana na mfululizo wa mauaji yanayofanywa na polisi katika shughuli za kisiasa za Chadema na mipango ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), kwa mbinu haramu, Kamati Kuu imezingatia masuala mbalimbali na kupitisha azimio la kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Lengo la barua hiyo ni kumshauri achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka yake na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, aunde tume huru ya kuchunguza vifo vyenye utata.”

Mbowe alisema iwapo Serikali haitazingatia ushauri huo, Chadema kitawaongoza wananchi kwa njia za kidemokrasia ikiwamo maandamano ya amani, kushinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kwa masilahi ya taifa.
Alisema Kamanda Kamuhanda na wenzake wanatakiwa kushtakiwa kwa kuwa tukio la mauaji ya Mwangosi lilitokea wakiwa eneo la tukio.

“Waziri Nchimbi ambaye ndiye anayesimamia jeshi hili pamoja na wenzake tunataka wawajibike au kuwajibishwa kwa kuwa wananchi wamekufa chini mikono ya askari polisi. Mkuu wa FFU wa Mkoa wa Morogoro na Kamanda wa Polisi Iringa nao walihusika kwa kuwa mauaji yalitokea wao wakiwa eneo la tukio,” alisema Mbowe.

“Kamati Kuu imejadili kwa kina mfululizo wa mauaji ya watu wetu ambayo hutokea kwenye mikutano na shughuli za Chadema. Vifo ni vingi lakini sisi tumeelekeza katika vifo vilivyotokea Arusha Mjini, Arumeru, Igunga, Singida, Morogoro na Iringa,” alisema Mbowe.

Alisema lengo la uchunguzi ni kutaka kupatikana kwa wahusika walioshiriki mauaji hayo bila kujali nyadhifa zao, ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kwa kuwa hilo ndilo litakalojenga msingi wa taifa kubaki katika hali ya amani.

..Yawatimua madiwani wake Mwanza
Chama hicho kimetangaza kuwavua uanachama madiwani wake wawili wa Mwanza, Adamus Changulani (Igoma) na Henry Matata (Kitangile) kwa madai ya kukiuka kanuni na maadili ya chama.

Mbowe alisema hatua hiyo imetokana na uchunguzi kubaini kuwa walitumiwa na Serikali pamoja na wale wa CCM, kushiriki katika tukio la kumwondoa aliyekuwa meya wa jiji la Mwanza.

“Suala la kuondolewa kwa meya kama taratibu zimefuatwa hakuna tatizo na hicho ndicho Chadema inachokipigania. Lakini hatua zilizochukuliwa dhidi ya meya wa jiji hilo hazikufuata taratibu na tulibaini kuwa viongozi wetu wamehusika. Tumechukua hatua bila kujali wadhifa wa wahusika,” alisema Mbowe.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz