Wednesday, September 12, 2012

JK Yuko Kenya Kwa Ziara Ya Kiserikali



 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na mwenyeji wake Rais Mwai E. Kibaki wa Kenya pamoja na ujumbe wake wakiingia Ikulu ya Nairobi  Jumanne, 11 Septemba , 2012,  alipoanza Ziara Rasmi ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu nchini humo.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na mwenyeji wake Rais Mwai E. Kibaki wa Kenya wakipata picha ya kumbukumbu  Ikulu ya Nairobi  Jumanne, 11 Septemba , 2012,  alipoanza Ziara Rasmi ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu nchini humo. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Mhe Bernard Membe na kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Profesa Sam K. Ongeri
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete  pamoja na ujumbe wake na wenyeji wao wakianza  Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete  pamoja na ujumbe wake na wenyeji wakiongea na wanahabari na kisha kupiga picha ya pamoja baada ya  Mazungumzo yao Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili.
 

.
PICHA NA IKULU

 =====================================================================
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini Kenya  Jumanne, 11 Septemba , 2012,  kuanza Ziara Rasmi ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu ikiwa ni ziara yake ya kwanza rasmi nchini humo ingawa ameshawahi kufanya ziara kadhaa za kikazi nchini Kenya.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Rais Kikwete ambaye amefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, amepokewa na mwenyeji wake, Rais Mwai E. Kibaki na kwa mbwembwe zote za kiprotokali zinazoambatana na ziara rasmi za kiserikali.
Baadaye mchana, Rais amekwenda Ikulu ya Kenya ambako ametia saini kitabu cha wageni, akafanya mazungumzo ya faragha na Rais Mwai Kibaki kabla ya kufanyika kwa Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili majirani na wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete na ujumbe wake amekwenda kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta ambako wamepokewa na Waziri wa Elimu ya Juu, Mheshimiwa Margaret Kamar, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Onesmus Mutungi na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Olive Mugendi.
Kwenye chuo hicho ambacho Desemba 8, mwaka 2008, kilimtunuku Rais Kikwete Shahada ya Uzamivu ya Heshima, amefungua rasmi Jengo la Shule ya Ukarimu na Utalii ya Chuo hicho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Shule hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utalii ni sekta muhimu sana katika chumi za nchi za Afrika Mashariki na ambayo mchango wake unagusa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wa nchi za ukanda huo.
Rais pia amesema kuwa nchi hizo za Afrika Mashariki sasa zimekuwa ni eneo lenye mvuto mkubwa katika nyanja ya utalii ambao unaweza kuwaingizia wananchi na mataifa ya Afrika Mashariki mapato zaidi kama changamoto zinazoikabili sekta ya utalii kwa sasa zitashughulikiwa ipasavyo na kwa pamoja na nchi hizo.
Miongoni mwa changamoto ambazo Rais Kikwete amezitaja ni ukosefu wa miundombinu ya kutosha kufanikisha kwa namna bora zaidi sekta ya utalii, ukosefu wa juhudi za pamoja kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo muhimu la utalii, na umuhimu wa kuboresha kiwango cha usalama wa watalii.
Aidha, Rais Kikwete amezielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na umuhimu wa kuwepo na viza ya pamoja ya utalii kwa nchi zote za Afrika Mashariki, kuwepo kwa safari za ndege za kutosha kutoka kwenye mataifa makubwa yanayozalisha watalii kwa wingi kuja Afrika Mashariki na umuhimu wa kupungua kwa nauli za ndege za kuja Afrika Mashariki.
Jioni, Rais Kikwete ametembelea Taasisi ya Utatifi wa Kilimo ya Kenya (KARI) ambako anatarajiwa kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Kenya, Mheshimiwa Dr. Sally J. Kosgei na usiku alikuwa mgeni rasmi kwenye Dhifa ya Kitaifa ambayo itaandaliwa na mwenyeji wake, Rais Mwai Kibaki.
Leo Jumatano 11 Septemba, 2012  Rais Kikwete ataweka shada la maua kwenye Kaburi la Mwanzilishi wa Taifa la Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, kwenye Viwanja vya Bunge la Kenya na kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha Brookside Diary kwenye Barabara ya Thika.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake, Rais Kikwete atatembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya (National Defence College) kilichoko Karen, Nairobi, ambako atapokelewa na Waziri wa Nchi wa Ulinzi, Mheshimiwa Yusuf Haji na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi.
Baadaye, Rais Kikwete atakwenda kutembelea Kituo cha Magonjwa ya Moyo na Kansa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ambako atapokelewa na Waziri wa Huduma za Matibabu, Mheshimiwa Anyang Nyong’o.
Baadaye jioni, Rais Kikwete, ambaye anaongozana na kundi kubwa la Wafanyabiashara wa Tanzania, atashiriki chakula cha jioni ambacho ameandaliwa na Jumuiya ya Wafanya Biashara ya Kenya.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Septemba, 2012