Kufuatia Utabiri wa Hali ya Hewa uliofanywa kwa pamoja na Mamlaka za Hali ya Hewa kwa nchi za Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki, Mamlaka ya Hali ya Hewa - Tanzania imetoa taarifa kuhusu uwezekano wa nchi kupata mvua nyingi iliyo juu ya wastani. Hali hii ya kuwa na mvua nyingi inatabiriwa kuikumba nchi kwa kipindi cha Oktoba, 2012 hadi Disemba, 2012 na huenda ikaendelea zaidi.
Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga). Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Septemba, 2012 katika mkoa wa Kagera na kaskazini mwa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu katika wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2012. Kwa ujumla mvua hizo zinatarajiwa kuwa juu ya wastani katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza ya mwezi wa Oktoba, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara). Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2012 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa).
Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2012 katika mkoa wa Kigoma na wiki ya pili ya mwezi Novemba katika mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Rukwa na Kigoma. Aidha maeneo mengi ya mikoa ya Katavi na Tabora mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma). Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Novemba na zinatarajiwa kuwa za juu
ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Novemba 2012 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mkoa wa Njombe na kusini mwa mikoa ya Mbeya na Morogoro. Maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa, mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Maeneo ya Kusini na Pwani ya Kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba, 2012 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Kwa kuzingatia hali hii Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa tayari imetoa taarifa/elimu kwa umma kupitia kipindi cha“Tuambie” cha TBC 1 na kuelekeza taasisi na wadau mbalimbali kuchukua hatua za tahadhari. Mfumo wetu wa kukabiliana na maafa una Kamati za Maafa kwenye ngazi ya mkoa, wilaya hadi kijiji ambazo zina majukumu ya kusimamia masuala ya maafa katika maeneo yao. Kamati zilizoanishwa hapo juu pamoja na wadau wote mnakumbushwa kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea. Katika jitihada za kujiandaa mnakumbushwa kuzingatia yafuatayo:-
1. Kutekeleza mipango mbadala katika maeneo mliyobaini kuwa yana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na mafuriko; kama vile kuhamisha wananchi maeneo ya mabonde kwenda sehemu salama na kurejesha mawasiliano endapo yataharibika.
2. Kupatikana dawa muhimu za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na madawa ya kusafisha maji ya kunywa (Water Guard Tablets).
3. Kupatikana kwa dawa muhimu za mifugo kwani magonjwa miguu na midomo (FMD) na homa ya bonde la ufa (RVF) yana uwezekano mkubwa wa kutokea.
4. Upatikanaji wa chakula cha kutosha. Aidha wananchi wahimizwe kuweka akiba ya chakula cha kutosha.
5. Kutenga fedha za kukabiliana na maafa endapo yatatokea.
6. Elimu kwa Umma itolewe kwa kuhusisha vyombo vyote vya mawasiliano na uongozi wa Vijiji na Mitaa.
7. Kuchukua hatua za ziada kwa maeneo ambayo yana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi.
8. Kuainisha mitaro inayoweza kuingiza maji katika migodi ya wachimbaji wadogowadogo, na kuchukua tahadhari zinazostahili.
9. Kuhakikisha kuwa mifereji na mitaro ya maji machafu kwa maeneo ya Jiji/miji iko safi na wazi wakati wote kupitisha maji.
10. Kuchimba au kukamilisha uchimbaji wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
11. Maofisa Ugani - Kilimo kutoa ushauri kwa wakati kuhusu mazao ya kupanda na pia wafugaji kutumia nafasi kuvuna malisho ya kutosha yatakayotumika kipindi cha kiangazi .
12. Kila ngazi kujiweka tayari kukabiliana na mafuriko ni muhimu kuunda timu za wataalam wa kukabiliana na athari zitakazotokea, majina yao yaainishwe na waelekezwe cha kufanya pindi hali ikiwa hivyo.
Ni matumaini yangu kuwa tukishirikiana katika kukabiliana na mvua nyingi pamoja na majanga yanayoambatana na mvua hizi, tunayo nafasi kubwa ya kujihakikishia usalama wa nchi yetu kutokana na majanga ya asili.
Nashukuru kwa ushirikiano wenu.
IMETOLEWA NA KATIBU MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU