Thursday, September 27, 2012

RAIS KIKWETE AMPONGEZA MBUNGE FILIKUNJOMBE,LEO AMWONA ADUI NEC



Rais Jakaya  Kikwete akimpongeza mbunge  wa Ludewa Deo Filikunjombe kwa  kutekeleza ilani ya CCM mara alipotembelea jimbo hilo mwaka jana 

Utendaji kazi wa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe, umemfurahisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisema kuwa utendaji kazi wa Filikunjombe ni utendaji wenye kasi ya kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wa Ludewa, katika Mkoa mpya wa Njombe. 

Akiwahutubia maelfu ya wakazi wa Kata ya Mawengi, hivi karibuni, Rais Kikwete alisema kuwa utendaji kazi wa Mbunge Filikunjombe ni ishara tosha kuwa wana CCM hawakukosea kumchagua mbunge huyo katika kura za maoni, “jambo lililopelekea wapinzani kumheshimu ambapo hawakujitokeza kumpinga Filikunjombe katika Uchaguzi Mkuu na hivyo kumfanya apite bila kupingwa”.
 
Aidha, Rais Kikwete alionyesha kufurahishwa zaidi na mikakati mizuri ya Mbunge Filikunjombe baada ya Filikunjombe kumweleza wazi vipaumbele vyake vikubwa viwili atakavyoanza navyo katika Wilaya ya Ludewa.
 
Filikunjombe alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na “kuhakikisha bara bara ya lami inaanza kujengwa Ludewa [ambapo toka Tanzania ipate uhuru wananchi wa jimbo la Ludewa hawajawahi kuiona lami] na pia kuhakikisha kuwa Uchimbaji wa Liganga na Mchuchuma unaanza mara moja”.
“Hamkukosea,” alisema Rais Kikwete huku akiwashukuru wananchi kwa kumchagua Deo Filikunjombe kuwa Mbunge wa Ludewa.
 
Pamoja na kupigania usafiri bora Ziwa Nyasa, Filikunjombe pia, amekuwa akipigania uwepo wa soko la uhakika kwa zao la mahindi kwa wakulima wa Ludewa, jambo lililopelekea serikali, mwaka huu, kununua mahindi katika vituo vya Mawengi, Ludewa Kijijini, Shaurimoyo na Mlangali. 
 
Rais Kikwete aliviunga mkono vipaumbele hivyo akisema kuwa ni vipaumbele vyenye tija katika maendeleo ya Wilaya ya Ludewa na kwamba ni azma yake yeye Rais Kikwete kuona kuwa juhudi zaidi zinaelekezwa katika wilaya hiyo. 
 
Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM taifa, amewataka wananchi wa Ludewa waendelee kushirikiana na Mbunge Filikunjombe kwani anaitekeleza vema ilani ya Chama Cha Mapinduzi. 
 
“Sasa ni zamu ya Ludewa kubadilika ki-maendeleo,” alisema Rais Kikwete akisisitiza kuwa serikali yake itaelekeza nguvu zaidi jimboni humo akiongeza kuwa, Ludewa imechelewa mno kupata maendeleo.
 
"Nitakuja tena Ludewa,” alisema Rais Kikwete ambaye pia aliwashukuru wananchi kwa kuwachagua madiwani wengi toka CCM. “Ludewa kuna madiwani 32 na kati ya hao ni Diwani mmoja pekee ametoka upinzani, huu ni ushindi mnono,” alisema Kikwete. 
 
 
Filikunjombe, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alimweleza Rais Kikwete kuwa pamoja na kwamba Taifa linasherekea miaka 50 ya Uhuru, wakazi wa Ludewa walikuwa bado hawajapata uhuru na kwamba, mwaka huu chini ya utawala wa Rais Kikweye, Ludewa ndo wanapata uhuru wao baada ya kuwa na uhakika wa barabara ya lami na kuanza kutekelezwa kwa miradi wa Liganga na Mchuchuma.
 
Rais Kikwete alikuwa wilayani Ludewa kufungua mradi wa umeme wa KW 150 uliotekelezwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la ACRA, Ubalozi wa Italia, pamoja na Jumuiya ya Ulaya.

Nimelazimika  kiurudia habari  hii hapa leo ili  kuona ni jinsi gani CCM inavyojitafuna  yenyewe rafiki  wa leo ni adui wa kesho ndani ya CCM.

Ni nani alitegemea  leo kama CCM chini ya mwenyekiti  wake  Rais Jakaya  Kikwete ingemuengua mbunge Filikunjombe na Mkono katika orodha  wa  wagombea  wa  wajumbe wa NEC wilaya katika uchaguzi ndani ya chama kwa utendaji  wao wabunge hao?

Ila pia naweza  kujifunza jambo ndani ya CCM hawapendi kabisa  uwe msemakweli ama mpambanaji  wa ufisadi  wanapenda  zaidi  kulindana na ndio  sababu ya akina  Filikunjombe ambao  walionekana wazuri kwa  kuungana na  wapinzani  kuorodhesha majina yao kwa  kutaka waziri Mkuu   ajiuzulu kwa kufumbia macho mafisadi leo  wamegeuka ni wapinzani ndani ya CCM.

Hivyo kwa mwendo  huu  ni vigumu kwa hata hao ambao  wamepitishwa  kuja kufanya  vizuri kwa maana ya  kuwatumikia  wananchi  kwa  kupinga ufisadi  zaidi ya kuendelea kunyamaza kimya huko mafisadi  wakiendelea  kupongezwa na kubembelezwa ndani ya CCM.

Hapa ndipo napo sema ni heri CCM kutokana na mwendo huu ikaa pumzika ili kujipanga upya badala ya  kuondolewa kwa aibu mwaka 2015 na upepo huu wa M4C  kiukweli CCM inajichimbia kaburi lake na kujiandalia mazishi kabla ya  kifo chake .

Binafsi napingana hata  mfumo  uliopo ndani ya CCM kwani  leo  tunashuhudia mwenyekiti ni Rais  wa nchi hivyo hata kama atakosea ni vigumu  kumkemea  kiongozi  wa nchi .

Ila  pia siungi mkono kabisa  watoto  wa wenyeviti  wa CCM Taifa na Rais  kupewa nafasi ndani ya CCM kwani  leo  tunashuhudia  CCM kuna makundi mbali mbali lipo kundi la Rais na mwenyekiti  wa CCM Taifa , lipo kundi la mtoto  wa Rais ambaye ni mjumbe  wa baraza kuu la UVCCM  sasa badala ya  kuvunja makundi hayo tunakazana  kuwaziba midomo akiwa  Nimrod Mkono na Deo Filikunjuombe .

Hata salama nzuri ya chama  iliyoasisiwa na baba wa Taifa  hayati mwalimu Julius Nyerere  ile ya  kidumu  chama cha mapinduzi !!! inavurugwa  sasa na  kuwa  Kigumu chama cha mapinduzi!!??

Haya  jamani  wana CCM hiyo ndio  CCM na akina Nape Nnauye na Dkt Jakaya  Kikwete ipo  siku litabaki jina huu ni mtazamo wangu