Sunday, September 23, 2012

Neno La Leo: Mfalme Mgonjwa... kutoka kwa Mjengwa



Ndugu zangu,
KUNA tunaokumbuka kisa cha mfalme simba na wanyama wenzake. Mfalme simba alipatwa na ugonjwa. Akabaki kibandani asiweze kutembea. Na njaa nayo ikamshika. Wanyama wengi walimtembelea mfalme kumjulia hali. Walikwenda akina pundamilia, twiga, swala na wengineo. Kila aliyeingia kibandani kwa mfalme hakutoka nje.

Mfalme simba katika kiu yake ya nyama akamtamani sana kobe. Ni kobe katika wanyama wote ambaye hakuonekana katika nyumba ya mfalme simba kumjulia hali. Simba akatuma ujumbe akilalamika; “Enenda ukamwambie kobe, nashangaa katika kuugua kwangu sijamwona kuja kunijulia hali”!

Ujumbe ukamfikia kobe. Siku moja kobe naye akaenda kumjulia hali mfalme simba. Hakufika mpaka iliko nyumba ya mfalme simba. Alisimama mbali na kutamka: “Ewe mfalme wangu simba, nimekuja kukujulia hali, waendeleaje na afya yako?”.

Mfalme simba akajibu: “Mbona salamu hizo unazitoa ukiwa mbali hivyo?”. Kobe akamjibu mfalme wake: “ Kuna jambo linanishangaza mfalme wangu, naona nyayo zote za wanyama zimeelekea kwako, lakini hakuna nyayo zinazorudi”!

Katika jamii yetu sasa kuna akina mfalme simba wagonjwa na wenye njaa ya nyama. Wamewatafuna twiga, swala, pundamilia na wengineo. Sasa wanawatamani akina kobe pia! 
Ndio, katika nchi yetu sasa kuna harakati za kimakundi. Tunaziona ndani ya chama tawala, tunaziona nje ya chama hicho. Kuna wenye kuongoza harakati hizo. 

Na Watanzania tulio wengi tumekuwa ni watu wa kupenda sana kutafuna maneno. Kuna mawili makubwa ambayo ni mapungufu yetu; mosi, hatuna misimamo, pili, tukiwa nayo hatuisimamii. 

Tunapenda sana kuzungumza tusichomaanisha na mara nyingi hatumaanishi tunachozungumza. Na Mtanzania haumizi kichwa kujiuliza; “ kwanini nizungumze”. Maana suala si unachozungumza, bali ni kwanini unazungumza. 

Na kwanini wananchi wanaonekana kukata tamaa na kukosa imani kwa kinachozungumzwa na viongozi wao. Ndio, kikubwa kinachokosekana hapa ni namna nzuri ya kuwasiliana na wananchi ili kuwafahamisha na labda kuwaelimisha juu ya kilichotokea. 

Watanzania wengi hawana taarifa muhimu kuweza kutafsiri matukio na kinachozungumzwa na viongozi wao. Ni ukweli kuwa Watanzania walio wengi wanaishi vijijini. Ni takribani asilimia 21 tu ya Watanzania wenye fursa ya kupata taarifa muhimu juu ya kinachoendelea katika nchi yao; ni kupitia magazeti, runinga na redio. Waliobaki asilimia sabini na tisa ya Watanzania ndio hao wa Manzese Dar es Salaam, Mwanjelwa Mbeya, Kihesa na Kilolo Iringa na kwingineko. 

Ni hawa wasio na taarifa za kutosha kutafsiri mambo na hata kufanya maamuzi yanayotokana na kuwa na taarifa (informed decisions). Ni asilimia 79 hii ya Wanzania wa Mwanjelwa , Kilolo na kwingineko wenye kuiweka Serikali madarakani kwa wingi wa kura zao.

Media, kwa maana ya ya wanahabari ndio walipaswa wajitoe kwenye vita vya kimakundi na kuwasaidia Watanzania hawa kupata taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi. 

Lakini miongoni mwa wanahabari hawa, kuna walioingia katika foleni ya kwenda kuwajulia hali wafalme wagonjwa. Wamejiingiza kwenye vita ya kimakundi. Wamelisahau jukumu lao, wamelisahau kundi kuu. Ni kundi lile la asilimia 79 ya Watanzania. 

Tunaziona nyayo za baadhi ya wanahabari zikienda kwa wafalme wagonjwa, hatuzioni nyayo zao za kurudia!
Wanahabari walipaswa kuwa daraja la kupitisha taarifa kutoka chini kwa wananchi kwenda juu kwa viongozi, na kinyume chake.

 Lakini, miongoni mwa wanahabari hao, wameamua kwa makusudi kulivunja daraja hilo. Ni kweli kuwa kila mwanadamu kwa namna moja au nyingine ananunulika, lakini kwa wengine, bei zao ni utu na heshima, basi. Wanasukumwa kufanya yale yenye maslahi mapana kwa taifa.
 

Na hilo ni Neno La Leo. ( Limechapwa pia kwenye Mwananchi, leo Jumapili)
Maggid,
Iringa
0788 111 765