Tuesday, September 11, 2012

MPANGO WA NMB FINANCIAL FITNESS WAWAFIKIA ZAIDI YA WANAFUNZI 45, 000



Benki ya NMB imewafikia wanafunzi 45,000 wa shule za msingi katika mpango wake wa kukuza uelewa wa maswala ya kifedha uitwao NMB Financial Fitness.

Mpango huo ulioanzishwa mwezi Mei mwaka huu, una lengo la kuwahamasisha wanafunzi kujiwekea akiba kwa kutumia huduma za kibenki wanapokua wakubwa.

 
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ligula wakijisomea jarida la NMB Financial Fitness katika utambulisho wa mpango huu uliofanyika katika shule hiyo mkoani Mtwara.

Meneja wa NMB kanda ya Kusini, Thomas Kilongo alisema katika taarifa yake kwamba, mpango huo umeshawafikia wanafunzi 1,800 wa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara katika kampeni ya utoaji elimu iliyoanza wiki iliyopita.

Kilongo aliendelea kusema, “wanafunzi hawa wamefundishwa namna ya kutunza fedha ikiwa ni maandalizi ya kujiwekea akiba wakiwa wakubwa. Ili kufanikisha ndoto zao , maandalizi yanatakiwa kuanza sasa na NMB inatoa mwanga wa namna ya kufikia malengo yao,”


 
Wanafunzi wa shule ya Msingi Maji Maji wakati wa utambulisho wa NMB Financial Fitness katika shule hiyo wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Wanafunzi waliopatiwa mafunzo hayo walionyesha hamasa ya kutaka kufahamu mambo mbalimbali yanayohusu benki.

Akizungumza katika utambulisho huo, mwanafunzi wa shule ya Liwale iliyopo mkoani Lindi Idrissa Ndumbaro aliishukuru benki ya NMB kwa elimu hiyo ambayo baadae itamwezesha kuwa na uelewa wa matumizi mazuri ya fedha pamoja na kujiwekea akiba.

 
Wanafunzi wa shule ya Msingi Njega iliyopo wilayani Nanyumbu Mkoa wa Lindi, wakijisomea jarida la NMB Financial Fitness katika utambulisho wa mpango huo.

Nae mwanafunzi Anna Daudi wa Shule ya Msingi Ligula alisema, alifurahishwa na vitabu vya watoto NMB Financial Fitness vinavyofundisha hadidhi juu ya kupanga matumizi ya fedha na mengine mengi.