Chelsea imekuwa timu ya kwanza kuichapa Arsenal katika mechi za ligi kuu ya Uingereza msimu huu baada ya kuwachapa 1-2 katika uwanja wao wa nyumbani,Emirates siku ya Jumamosi.
Vijana wa Roberto Di Matteo ndio walikuwa wa kwanza kufunga katika dakika ya 20 kupitia mshambulizi Fernando Torres baada ya mkwaju wa adhabu kupigwa na Juan Mata.
Kiper wa Arsenal Vito Mannone afungwa
Na katika dakika ya 52 ya kipindi cha pili, Mata alipiga mkwaju mwengine wa adhabu ambapo ulimshinda mlinzi Laurent Koscielny na badala yake kumgonga mguu na kuingia ndani huku ikimuacha Kiper wa Arsenal Vito Mannone hoi.Lakini katika dakika ya 42 mshambulizi Gervinho alifunga bao safi hivyo kuzifanya timu hizo mbili ziende mapumzikoni zikiwa sare ya 1-1.
Wenger amekua akilalamika kwamba safu yake ya nyuma imekuwa ikizembea katika mipira ya adhabu.
Licha ya kufungwa huko, Arsenal walitawala ngoma hiyo nzima ya Jumamosi lakini safu ya mbele ya vijana hao wa Arsene Wenger iliyonekana kukosa makali na kuwa na kukosa umakini.
Man City waitafuna Fulham
Dzeko aifungia Man city bao
Mshambuliaji Edin Dzeko aliirudishia Manchester City heshima baada ya kufunga bao dakika moja tu baada ya kuingia uwanjani na kuwawezesha vijana wa Roberto Mancini kuichapa Fulham katika uwanja wao siku ya Jumamosi.
Kabla ya bao hilo la Dzeko, Fulhama na Man City walikuwa nguvu sawa ya 1-1.
Fulham ndio walikuwa wakwanza kupata bao katika dakika ya 10 kupitia mkwaju wa penalti. Bao hilo la penalti lilifungwa na Mladen Petric baada ya mlinzi wa Man City Pablo Zabaleta kumchezea visivyo mshambulizi wa Fulham John Arne Riise.
Hata hivyo kama sio kipa wa Fulham Mark Schwarzer vijana wa nyumbani wangelitota kwa mabao zaidi kwani aliokoa mikwaju mingi kutoka kwa Sergio Aguero, Mario Baloteli na Samir Nassir.
Kukiwa kumesalia dakika chache mpira kumalizika, mlinzi wa Man City alipiga krosi safi iliyoanguka karibu na miguu ya Dzeko ambaye hakupoteza nafasi hiyo na kufunga bao.
Liverpool yaifunza Norwich
Suarez afunga mabao matatu
Mshambuliaji matata wa Liverpool, Luis Suarez amefunga magoli matatu kati ya matano dhidi ya mawili ya Norwich, ukiwa ni ushindi wa kwanza kwa timu ya Liverpool katika msimu huu wa ligi kuu ya England.
Suarez alifunga goli la pili akiwa nje ya eneo la hatari baada ya kumiliki mpira akielekea lango la Norwich.
Suarez alifunga bao la tatu baada ya ushirikiano mzuri na Nuri Sahin.
Nohodha Steven Gerrard alishindilia msumari wa mwisho katika jeneza la Norwich kwa kufunga bao la tano na kuifanya timu hiyo kuangukia sasa nafasi ya 14 kati ya timu 20 za ligi kuu ya premier.
Kileleni wapo Chelsea wenye pointi 16.