Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Shaif Hamad akizungumza na wahanga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu huko ofisi kuu ya Chama hicho Mtendeni.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Shaif Hamad akizungumza na wahanga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu (hawapo pichani) huko ofisi kuu ya Chama hicho Mtendeni.
Mbunge wa Jimbo la Mtoni (CUF) Mhe. Faki Haji Makame akizungumza kwa niaba ya waganga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu, mbele ya Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto). Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
----
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amelaani kitendo cha vyombo vya dola kuwapiga na kuwakamata wafuasi wa chama hicho na kuwaacha wa vyama vyengine na askari waliojeruhi raia wasio na hatia, siku ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu Septemba 16 mwaka huu.
Akizungumza na wahanga wa tukio hilo huko Makao Makuu ya CUF Mtendeni mjini Zanzibar jana, Maalim Seif alikiita kitendo cha askari hao kuwa ni cha kibaguzi kinachoweza kuathiri hali ya maelewano inayoendelea kudumu Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alisema jukumu la vyombo vya dola ni kusimamia haki kwa raia na si kuwabagua, kama walivyofanya wakati wa uchaguzi mdogo wa Bububu, ambapo wafuasi wa CUF peke yao ndio waliopigwa na kukamatwa, wakati viongozi na wanachama wa vyama vyengine walihusika wazi wazi katika vurugu hizo.
“Bila shaka huu ulikuwa mpango wa kupangwa, wanachama wa vyama vyengine hawakuchukuliwa hatua yoyote, hata Mbunge hakuheshimiwa na alipigwa kwa sababu tu anatoka CUF”, alisema Maalim Seif.
Alieleza kuwa katika mazingira ya amani na maelewano yaliyopo Zanzibar haikutarajiwa baadhi ya viongozi wa serikali na wa CCM kusimamia askari wa vyombo vya dola, wakiwemo walioficha nyuso zao kwa kuvaa ninja kuwapiga na kuwakamata wananchi wasiokuwa na makosa kwa njia ya kibaguzi.
Katika vurugu hizo wafuasi 22 wa CUF akiwemo Mbunge wa CUF jimbo la Mtoni, Faki Haji Makame walikamatwa na wengine kujeruhiwa vibaya, katika harakati za uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, ambapo mgombea Uwakilishi wa CCM alitangazwa kuibuka mshindi.
Wakati huo huo, Mbunge wa jimbo la Mtoni Faki Haji Makame amemshitaki Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai na askari Polisi wa kituo cha Bububu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema. Mbunge huyo analalamikia vitendo vya vya uonevu alivyofanyiwa wakati wa harakati za uchaguzi mdogo wa Bububu na baadaye kubambikiziwa kesi.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar ya Septemba 19, ambayo nakala zake zilitumwa kwa Mkuu wa Polisi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mbunge huyo alisema Vuai alishirikiana na vijana wa CCM waliokuwa wamewekwa tawi la CCM Bububu na baadhi ya Polisi kumwita kihadaa kumpiga na baadaye kumfungulia mashitaka.
“Wakati nikienda kuwatembelea jamaa zangu kule Bububu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar aliniita, nilipofika akawaleta vijana wa CCM wakanipiga ngwara na nilipowaita Polisi walikuja kunichukua na kunifungulia mashitaka ya kupigana hadharani”alilalamika Mbunge Makame.
Hata hivyo alisema anashangazwa na kitendo cha Polisi kuwaacha vijana hapo pamoja na Vuai walioshiriki kumpiga na sasa hajui anashitakiwa kupigana na nani. Katika barua hiyo aliyoituma jana, alieleza kuwa vijana hao baadhi yao walikuwa na vipande kadhaa vya kupigia kura waliachiwa na Polisi kupotea na wala hawana kesi wakati yeye na wafuasi wengine wa CUF waliteswa na kufunguliwa kesi.
Mbunge huyo anamtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Zanzibar kuchunguza kwa kina tukio hilo, kufuatia malalamiko ambayo tayari ameshayawasilisha huku akiendelea na taratibu za kuwasiliana na wanasheria wake kusimamia kesi hiyo.
Mbunge huyo alieleza kuwa ana wasiwasi askari Polisi Zanzibar wanashirikiana na viongozi na wafuasi wa CCM kukiuka taratibu za kazi zao za kusimamia haki kwa raia wote.
Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad leo anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa CUF huko katika viwanja vya Kwa Geji Bububu, ikiwa ni mkutano wa kwanza tokea kufanyika uchaguzi huo mdogo.
Maalim Seif alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani na Uingereza, wakati uchaguzi huo ulipofanyika, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, marehemu Salum Amour Mtondoo.
Na
Hassan Hamad
Of isi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar