Thursday, September 13, 2012

‘HAKUNA WA KUMWONDOA MUFTI SIMBA KWA NGUVU’.



 
Mufti wa Tanzania Sheikh Issah Bin Shaaban Simba. 
Na Datus Boniface.
Wakati kundi kubwa la waumini wanaodaiwa kuwa ni wa dini ya Kiislam wakipanga kufanya maandamano makubwa kwa ajili ya kumwondoa kwa nguvu Mufti wa Tanzania, Sheikh Issah Bin Shaaban Simba, jeshi la Polisi limesema hakuna mwenye ubavu wa kufanya hivyo.
Pia,jeshi la  Polisi limesema hakuna mwenye ubavu huo siyo kwa kumng’oa Mufti bali pia kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta) Dkt.  Joyce Ndalichako, kwani wamewekwa kwa taratibu na sheria.
Hivyo, kuna taratibu na sheria maalum ambazo zinaweza kufuatwa kwa lengo la kuwaondoa, lakini siyo kundi la waumini au wanasiasa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova ameonya kuwa kundi lolote la kidini au kisiasa lenye adha hiyo halitavumiliwa.
“Ni lazima ifahamike wazi kuwa jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua madhubuti za kisheria pale ambapo kundi lolote la kidini, la kisiasa au taasisi itakapobainika kuhatarisha usalama wa Wananchi wasio na hatia”alisema
Hata hivyo Kamanda Kova amewahakikishia uongozi wa BAKWATA kuwa, jeshi la Polisi lipo makini, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa hivyo litakabiliana kikamilifu na kundi dogo au kubwa litakalojaribu kuvamia ofisi hiyo.
Aidha, amesema maandamano ambayo siyo rasmi ambayo hayana kibali ni marufuku kufanyika na kundi lolote la dini au kisiasa.