Thursday, September 27, 2012

Bodi mpya ya Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar(ZSTC) Yazinduliwa



Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui akitoa hotuba ya Uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa ZSTC huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar jana.
  Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZSTC Kassim Malik Suleiman akitoa hotuba ya Shukrani na kuomba ushirikiano kwa wajumbe hao huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar jana
   Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui kulia akimkabidhi Zawadi Mwenyekiti wa Zamani wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZSTC Mwinyiuwesa Idarous Yussuf huko katika Uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa ZSTC katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar.
   Baadhi ya Wajumbe wa Bodi Mpya na yazamani wakiwa katika Kikao cha Uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa ZSTC huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar
  Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui (wakatikati)akiwa katika Picha ya Pamoja na Bodi mpya ya Wakurugenzi wa ZSTC huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar. Picha zote na Yussuf Simai, Maelezo
--
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kufanya mapinduzi ya zao la Karafuu kwa lengo la kukuza pato la nchi na wakulima wa zao hilo ili kuondokana na umasikini.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmeid Mazrui wakati alipokuwa akizindua bodi mpya ya Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar(ZSTC) katika Ukumbi wa Hoteli ya Ocean View nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
 
Amesema kutokana na sheria utaratibu na uongozi mpya wa shirika hilo utaweza kuufanya mabadiliko mengi na makubwa ili kuona zao la karafuu linabaki kuwa moja ya vianzio vya uingizaji wa fedha za kigeni na puia kuleta taifa kwa wananchi.

Mazrui amesema anamatumaini na Bodi mpya ya ZSTC na kwamba itajitahidi kuziba mianya yote ya uuzaji karafuu kwa njia ya magendo na kuwashajihisha wananchi kuliuzia shirika hilo karafuu zao.
 
Ameongeza kuwa juhudi za makusudi zitafanywa kuona kila mkulima anafaidika na mazao yake ambapo pia Wizara yake itaendelea kuhimiza upandaji wa mikarafuu kwa lengo la kulienzi na kulikuza zao hilo.
 
Amewataka wananchi kuendelea kulitunza zao hilo kwavile ndio njia itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Waziri Mazrui ameihakikishia mashirikiano ya karibu Bodi hio ili kuona inaleta tija na kuitaka kusimamia sheria mpya ya shirika hilo. 
 
Mapema Katibu mkuu wa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Julian Banzi Raphael amesema hivi sasa ulimwengu wa biashara unabadilika kwa kasi kubwa hivyo hakuna budi Shirika la ZSTC kwenda na wakati ili lisibaki nyuma kibiashara .
 
Aidha Julian alisisitiza Bodi mpya kubuni mbinu ambazo zitaweza kukidhi haja ya wakati uliopo licha ya changamoto nyingi ambazo zinaikabili Shirika hilo. 
 
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa ardhi kwa ajili ya upandaji wa Mikarafuu mipya hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni nchi ya Visiwa ambavyo ardhi yake imekuwa ikipungua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
 
Bodi hiyo mpya ambayo itadumu kwa miaka mitatu inaongozwa na Maalim Kassim Suleiman na itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa Shirika la Biashara la Zanzibar ZSTC linaimarika zaidi kiutendaji.
 
IMETOLEWA NA
Fakih Mbarouk
 MAELEZO ZANZIBAR