Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Dk. AshaRose Migiro akiongea na waandishi wa habari
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Hawa Ghasia , akiongea wakati wa mkutano huo
Idd Uwesu, Arusha Yetu
Baraza la Viongozi Wakuu wa Serikali za Mitaa la Afrika Mashariki (EALGF) limezinduliwa rasmi jijini Arusha huku viongozi hao wakitakiwa kulitumia baraza hilo kikamilifu ili kutoa mchango mkubwa wa maendeleo endelevu ya wananchi wa nchi wanachama ambao wanawahudumia
Baraza hilo lililoundwa kutokana na maazimio ya Mkutano wa nchi wanachama uliofanyika huko Kigali Rwanda mwaka jana limezinduliwa na Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Dk. AshaRose Migiro.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo Dk. Migiro amesema kuwa serikali za mitaa kama mdau wa karibu wa wananachi katika mifumo ya tawala za nchi zinalo jukumu kubwa la kuahakikisha zinatoa huduma nzuri kwa wananchi wao hivyo uwepo wa baraza hilo utazisaidia kuja na mikakati iliyobora zaidi katika kutekeleza majukumu yao.
Nae waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, amesema baraza hilo limedhamiria kuwawezesha viongozi wenye dhamana hiyo kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha utendaji wa Serikali za Mitaa na utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa Umma, kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika kanda ya Afrika Mashariki.
Kupitia mkutano huu pia viongozi hawa watapata nafasi nzuri ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya uwakilishi wa wananchi unavyofanyika, kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vyombo vya Uwakilishi wa wananchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Nchi za Visiwa vya Comoro na Sudan ya Kusini pamoja na wadau wengine wa maendeleo kama Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) wakialikwa kushiriki.