Saturday, August 18, 2012

WATU WATATU WAPOTEZA MAISHA KATIKA MATUKIO YA AJALI MKOANI DODOMA


Na. Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma
. Watu watatu wamepoteza maisha  baada ya kupatwa na  ajali katika matukio matatu tofauti ya ajali za usalama barabarani mkoani Dodoma hivi karibuni.
Akizungumzia tukio la kwanza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen alisema lilitokea tarehe 09 agosti, majira ya saa 18:45 hrs jioni katika eneo la Mbande Wilaya ya Kongwa katika barabara kuu ya Dodoma/Morogoro.
Alisema katika tukio la ajali hiyo Gari namba T.668 ATC Mitsubishi Fuso iliyokuwa ikiendeshwa na Dereva Arlon John Mkazi wa Babati liliigonga PikiPiki namba T.886 BWL aina ya FELKON.
“Chanzo cha ajali hii ni dereva wa pikipiki akitokea Barabara ndogo aliingia barabara kubwa ya Dododma / Morogoro bila kuwa makini na kusababisha gari hiyo MITUSUBISH FUSO kumgonga na kumsababishia kifo papo hapo.” Alieleza Kamanda Zelothe
Bw. Zelothe Stephen alimtaja marehemu wa ajali hiyo ambaye ni dereva wa pikipiki kwa jina la Edward Semundi mwenye umri wa miaka (29) Mgogo na mkazi wa kijiji cha Marungu.

Aidha katika ajali nyingine Bw. Zelothe alisema ilitokea siku ya alhamisi agosti 08, mwaka huu katika kijiji cha Manyata huko wilayani Kongwa, Majira ya saa sita na nusu usiku iliyohusu ajali ya gari kupinduka na kusababisha kifo.
Ajali hii ilihusisha Gari namba T.599 AZH aina ya MiTSUBISH CANTER iliyokuwa ikiendeshwa na Dereva ambaye hakufahamika mara moja kwani baada ya ajali hiyo alikimbia kusikojulikana na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.
Alimtaja marehemu katika ajali hiyo kuwa ni abiria aliyekuwa katika gari hiyo aliyefahamika kwa jina la Martha Senyagwa mwenye umri wa miaka (30) mkaguru na mkazi wa kijiji cha Ndaribo Wilayani kongwa.
 Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi aliokuwa akiendesha Dereva huyo Kumfanya kushindwa kulimudu gari lake na kusababisha gari hilo kuacha njia na kupinduka kisha kusababisha kifo.
Katika Tukio la tatu la ajali mkoani Dodoma Mkuu huyo wa Polisi alisema lilitokea mnamo tarehe 08 agosti mwaka huu majira ya saa moja kamili usiku, katika kijiji cha Kungugu Wilaya ya Bahi Katika Barabara itokayo Dodoma kuelekea Manyoni.
Kamanda Zelothe alisema, gari namba IT 3123 aina ya TOYOTA YATZ iliyokuwa ikiendeshwa na Dereva Ally Ramadhani mwenye umri wa miaka (56) Mnyamwezi na mkazi wa Kimara Baruti Jijini Dar es Salaam ilimgonga mtembea kwa miguu na kumsababishia kifo chake palepale.
Alimtaja marehemi kuwa ni Mosi Yohana mwenye umri wa Miaka (40) Mgogo na mkulima wa Kijiji cha Kungugu ambaye alikuwa anavuka barabara toka  upande wa kushoto kwenda kulia.
Bw. Zelothe alisema Chanzo cha ajali hii ni uzembe wa Dereva kutokuwajali watembea kwa miguu, Kwani alidai Madereva wamefundishwa sheria za Usalama Barabarani kuliko Raia wa kawaida hivyo anapaswa kuwa makini kwa watumiaji wa barabara.
“Dereva kwa kutumia taa za gari analoliendesha ana uwezo na  upeo wa kuona umbali wa mita mia tatu mbele yake, hivyo akiwa makini kwa mazingira haya anaweza kuepukana na ajali zisizo za lazima” aisisitiza Bw. Zelothe
Dereva aliyesababisha ajali hiyo amekamatwa na atafikishwa mahakamani kijibu mashtaka yanayomkabili.