Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Kamati
Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi imejadili majina ya
wanachama watatu wanaowania kuteuliwa na Chama hicho kwa ajili ya
kinya’nganyiro cha Uchaguzi mdogo wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi
Jimbo la Bububu.
Taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, ilisema kwamba kikao hicho kimependekeza kwa Kamati Kuu ya CCM
majina ya Husein Ibrahim Makungu (Bhaa), Omar Ibrahim Kilupi na Fatma Salim Said.
“Kikao kilipokea na kujadili majina ya wana CCM 3 walioongoza katika kura za maoni kwenye
mkutano mkuu maalum wa Matawi ya Jimbo la Bububu na hatimaye kutoa
mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kwa hatua za mwisho” Ilisema taarifa hiyo ya CCM.
Katika
hatua nyengine, Kamati Maalum imempongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia vizuri kazi ya uokoaji katika ajali ya kuzama kwa Meli ya Skagit, iliyozama Julai 18 karibu na Kisiwa cha Chumbe Kusini mwa Kisiwa cha Yasin.
Katika ajali hiyo, watu 150 waliokolewa wakiwa hai huku wengine zaidi ya mia moja wakipoteza maisha. Meli
ya Mv. Skagit ilibeba abiria 290 ikitokea Bandari ya Dar es Salaam
kuelekea Bandari ya Malindi Zanzibar,ilizama majira ya saa saba mchana.
Wajumbe wa Kamati Maalum pia
wamempongeza Rais Dk. Shein, kwa hatua aliyochukua ya kuiangiza Wizara
ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuhakikisha
inatafuta fedha haraka kwa ajili ya kuanunua meli ya abiria na mizigo.
“Kikao
pia kimempongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa hatua
aliyochukua ya kumuagiza Waziri wa Fedha wa Serikali (SMZ), kutafuta
fedha haraka iwezokanavyo, kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya ya kubebea
abiria na hivyo kuwaondolea wananchi tatizo la usafiri wa majini
lililodumu kwa muda mrefu sasa” Ilisema taarifa hiyo ya CCM ZanzĂbar.
Aidha,
Kamati Maalum imefarijika na hatua ya Rais Dk. Shein kuagiza ununuzi wa
meli mpya ambayo itasaidia kuondoa tatizo la usafiri na usafirishaji
kwa wananchi.
“Kikao
kimesema kauli hiyo ya Mhe. Rais wa Zanzibar ya kutafuta meli sio tu ni
ya kijasiri, bali pia imetolewa wakati muafaka, ambapo Serikali imethubutu
kupunguza kutoka Bajeti yake ya mwaka 2012/2013, jumla ya Tshs. Bilioni
17, ikiwa ni kianzio cha fedha za kununulia meli hiyo” Iliongeza
taarifa hiyo ya CCM.