Kwa maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na
pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza
kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa
hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi
huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge
pamoja na udhaifu wa serikali.
Ukiondoa tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama
kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia
kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani
uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge
kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
Hivyo hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na
kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye
wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya
kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya
wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua
za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye
watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo,
Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha
misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.
Hata baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza
kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia
serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya
nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa
haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe
15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.
Nilisema bungeni kwamba “Naamini iwapo maazimio ya Bunge
juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC
yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta
ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio
kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa
ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa uzito
unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii
mara kwa mara”.
Mathalani, Waziri wa Nishati na Madini ameeleza bungeni
tarehe 28 Julai 2012 kuwa wapo wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye
kulihujumu Shirika la Umeme (TANESCO) na Spika wa Bunge akahitimisha kuwa
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itachunguza tuhuma husika na pia
kwamba inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za Maadili (Code of Conduct) ili
kudhibiti hali hiyo.
Hata
hivyo, Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka 2008 baada
ya Kashfa ya Richmond iliazimiwa katika Azimio Na. 11, kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya
Mwaka 1995 (The Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe
marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa
Viongozi Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi
wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze
rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje ya Bunge
kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”
Bunge
lilitaarifiwa Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba kikundi kazi
(Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye mapendekezo ya
kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura 398) ambao ulikuwa
katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge
lilielezwa kuwa serikali ilitarajia kuwasilisha muswada husika katika mkutano
wa kumi na tisa wa Bunge la tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la
tisa kama ilivyoshauriwa na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu
azimio hilo halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.
Aidha, kumetolewa madai ya baadhi ya wabunge kupokea ama
kudai rushwa suala ambalo nalo Spika wa Bunge ametoa uamuzi kuwa
litashughulikiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Lakini
Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si mara ya kwanza
kwa tuhuma za namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa kamati mbalimbali
za bunge.
Hata hivyo, kwa sababu ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa
ukamilifu tuhuma kama hizo zitaendelea kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa
kamati ya bunge ya nishati na madini. Izingatiwe kwamba madai ya rushwa
kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza kuhusu Kamati ya Nishati na Madini na
binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena kwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza
uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili
ya kupitisha bajeti bungeni mwaka 2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi
wabunge kwa rushwa hata hivyo hatua hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa
au kuwachukulia hatua wahusika.
Suala hili likatajwa tena na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
David Kafulila kuhusu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na likatajwa tena
na Kiongozi wa Upinzani Freeman Mbowe na Mbunge wa Kyela Dr Harrison Mwakyembe
kuhusu uchaguzi wa Afrika Mashariki lakini hatua hazikuchukuliwa kuchunguza
wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo maazimio kuhusu uhalali wa
utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya
kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 (Maarufu kama Sakata la Jairo), yangetekelezwa na wahusika
wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu pia kwa watendaji wa wizara na mashirika
ya umma kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yenye kulenga
kuwaathiri wabunge kwa rushwa na maslahi mengine ya kifedha.
Katika hali inayoonyeha kwamba Serikali bado haioni uharaka
na ulazima wa kuchukua hatua, wakati bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28
Julai 2012 kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi
kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo
ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa bungeni toka
yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011; lakini Waziri akajibu tu kwamba hawezi
kufanyia kazi taarifa za magazetini, bila kujali kwamba nilichouliza hakihusu
taarifa za magazetini bali maazimio ya bunge baada ya kazi iliyofanywa na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge
ambayo ilihoji wahusika na kupata pia vielelezo.
Kwa hiyo, ni muhimu Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea
kwenye Hotuba niliyowasilisha bungeni na kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais,
Waziri Mkuu na Spika wa Bunge juu ya masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na
kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa
wabunge kuhusu suala la ununuzi wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO
nilieleza pia masuala mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu
mabilioni ya shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta na gesi
asili pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa kuchukuliwa.
Nimetoa maoni hayaleo jumapili tarehe 29 Julai 2012:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini