Tuesday, July 31, 2012

ADAM NDITI KUITWA ILI KUCHEZA DHIDI YA NIGERIA

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya umri wa chini miaka 20, Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen amesema atakihimarisha kikosi chake kabla ya mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya vijana Mataifa ya Afrika kwa kumjumuisha kiungo wa timu ya Mabingwa wa Ulaya, Chelsea, Adam Nditi.
Michelsen alisema kuwa taratibu za kumpata mchezaji huyo zimeanza kufanywa na Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF).
Michelsen alisema, Nditi ambaye anacheza beki wa kushoto au winga wa kushoto atakuwa chachu ya kuivisha timu hiyo inayohitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili kufuzu hatua inayofuata.
Mbali ya Nditi, kocha huyo pia alisema ana matumaini makubwa kuwa mshambuliaji wake, Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe.
Alisema kuwa Ulimwengu alipangwa kuja nchini kwa ajili ya mechi hiyo, lakini dakika za mwisho alihairisha safari hiyo na kuifanya kikosi chake kukosa umakini mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
"Najua kuwa tuna kazi kubwa mchezo wa marudiano, tunahitaji ushindi si chini ya mabao 2-0 na kuendelea, lazima tuhimarishe kikosi ili kuweza kufikia lengo letu," alisema Michelsen.
Wakati huo huo, Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) limesema kuwa litawasilisha malalamiko yao CAF kupinga hatua ya TP Mazembe kumzuia Ulimwengu kuichezea timu yake ya taifa.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa walifuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu.
Source:Mwananchi