Saturday, March 17, 2012

MCHAKATO WA UNUNUZI WA VITABU KWA KUTUMIA FEDHA ZA FIDIA YA RADA



MAELEZO JUU YA MCHAKATO WA UCHAGUZI NA UNUNUZI WA VITABU
VITAKAVYONUNULIWA KWA KUTUMIA FEDHA ZA FIDIA YA RADA (BAE SYSTEM)


1.0     MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VITABU

1.1     Utangulizi

Katika jitihada za kupata vitabu bora vya kutumika kama vitabu vya
kiada katika shule za msingi, Menejimenti ya Wizara ya Elimu na
Utamaduni iliunda kikundi kazi cha maafisa tisa (9) ili kitoe
mapendekezo ya jinsi ya kufanya uchaguzi wa vitabu hivyo kutoka orodha
ya vitabu vingi ambavyo vilitumika awali.  Kikundi kazi kilitoa
mapendekezo ya matumizi ya vitabu viwili kwa kila somo na kila darasa
badala ya vitabu vingi.

1.2     Mchakato wa uchaguzi wa vitabu: -

Katika mchakato wa kuchagua vitabu bora vya kutumika kama vitabu vya
kiada katika shule za msingi.  Hatua zifuatazo zilihusika: -

i.      Vitabu vitakavyochaguliwa ni lazima view vimepata ithibati ya EMAC.
ii.     Wachapishaji wote waliwasilisha vitabu vyao vyote
vilivyothibitishwa katika Sekretarieti ya EMAC.
iii.    Baada ya kuwasilishwa vitabu vyote viliondolewa alama za
utambulisho wa mchapishaji (Publisher's identity) na wachapishaji
wenyewe.
iv.     Baada ya kujiridhisha kuwa vitabu vyote vimeondolewa alama za
utambulisho, vitabu hivyo vilipewa namba ya siri ya utambulisho.
v.      Wakaguzi wa Elimu wa Kanda/Wilaya waliteua walimu wa masomo
mbalimbali kutoka katika shule za Msingi na kuwasilisha orodha ya
majina Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
vi.     Katibu Mkuu Wizara ya Elimu aliteua majina machache kutoka katika
orodha i.e. walimu watatu kwa kila somo kwa kutumia vigezo vifuatavyo:
-

•       Uzoefu wa mwalimu katika kufundisha somo husika.
•       Jinsia (gender).
•       Kuangalia ulinganifu katika kanda/wilaya zote.
•       Walimu wasiwe na 'interst' katika uchapaji wa vitabu.
•       Mwalimu wa darasa wakati wa uchaguzi.
•       Ngazi ya Elimu ya mwalimu i.e diploma, digrii n.k.

vii.    Timu ya usimamizi "Supervisor's team" ilichaguliwa ikiwa na
wajumbe wafuatao: -
•       Waendelezaji wa mitaala – 2
•       Wakaguzi wa shule za msingi waliostaafu – 2
•       Mwalimu kutoka chuo cha ualimu – 1
•       Mkufunzi kutoka chuo kikuu – 1
•       Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Elimu ya Msingi - 1

viii.   Uchaguzi ulifanywa kwa kutumia kifaa cha kufanyia uchambuzi wa
vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu ambacho kiliwekewa vigezo
mbalimbali.
ix.     Baada ya uchambuzi kukamilika orodha ya vitabu vilivyoteuliwa
iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa
hatua zaidi.

Uchambuzi tajwa hapo juu uliwezesha kupatikana kwa vitabu viwili
katika kila somo na katika kila darasa kwa shule za awali na shule za
msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

1.3     Uchambuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA)

Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ilifanya  uchambuzi wa
kina katika mchakato mzima wa uchaguzi wa vitabu na kuridhika na hatua
zote za mchakato huo.  Hata hivyo, PPRA walitoa msisitizo kuwa, kamati
ya Ithibati ya Taifa (EMAC) ibaki na jukumu lake kuu la kutoa ithibati
kwa aina ya vitabu na wachapishaji wa vitabu (Book standards, titles
and publishers approval).

2.0     Mchakato wa ununuzi wa vitabu

Mchakato wa ununuzi wa vitabu utafanyika kwa kufuata Sheria ya Ununuzi
wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yaliyofanyika mwaka
2011, pamoja na Kanuni zake Tangazo la Serikali Na. 97 la mwaka 2005.



2.1     Ununuzi wa Vitabu vya Kiada na Kiongozi cha Mwalimu: -

Ununuzi wa vitabu vya kiada na viongozi vya walimu utazingatia aina ya
vitabu vilivyochaguliwa na WEMU kwa kila darasa kama ilivyoainishwa
katika Waraka wa Eimu Na. 2 wa Mwaka 2010. Waraka unaainisha vitabu
viwili vilivyoteuliwa kwa kila darasa na usambazaji wake kufanyika
katika mfumo wa Kanda (Kanda ya Mashariki na Magharibi). Kutokana na
mgawanyo huu, kila Mchapishaji atauza vitabu vyake kwa takribani mwaka
mmoja katika Kanda moja na kuhamia Kanda nyingine katika mwaka
unaofuata.  Hata hivyo, kwa kuwa ununuzi kwa kutumia fedha za BAE
Systems unafanyika mara moja, ununuzi utazingatia vitabu vyote vya
Wachapishaji kwa mgawanyo wa Kanda zilizopo.

Utaratibu utakaotumika katika ununuzi huo ni wa kununua kutoka kwa
mzabuni mmoja tu "Single Source".  Hii ni kulingana na Kanuni namba
69(1)(a & (f).  Sababu za kufanya ununuzi wa vitabu kwa kutumia
utaratibu wa kununuz kutoka kwa mzabuni mmoja ni: -

1.      Vitabu viwili vya Kiada na Kiongozi cha Mwalimu vilivyothibitishwa
na Kamati ya Ithibati ya Taifa (EMAC) kwa ngazi ya Shule za Msingi
viliteuliwa kwa kila somo na kila darasa na Wachapishaji wake pia
wameteuliwa na kuthibitishwa na EMAC.

2.      Hapo awali vitabu viliweza kununuliwa kutoka kwa wauzaji
"booksellers" na wasambazaji "distributors" ambapo utaratibu huo
ulitawaliwa na udanganyifu mkubwa "book piracy" uliosababisha vitabu
kutokuwafikia walengwa.

Kwa utaratibu wa kununua moja kwa moja kutoka kwa wachapishaji
"Publishers", Serikali imekusudia kuepukana na matatizo mbalimbali
yaliyokuwa yanatokea nyakati za awali kwa sababu mchapishaji atatakiwa
kufikisha vitabu moja kwa moja katika shule husika

3.      Utaratibu wa kununua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa vitabu
utatusaidia kupata punguzo la bei na gharama za usambazaji kwani
tutakuwa na fursa ya kufanya majadiliano na makubaliano na mzabuni
husika, na kupata vitabu vingi zaidi.


2.2     Mchakato wa ununuzi wa Mihtasari na Kiongozi cha Mwalimu

Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ndiyo inalo jukumu la kuandaa mitaala
na kuisambaza kwa watumiaji kama ilivyoainishwa katika Sheria Na. 13
ya mwaka 1975 inavyoundaa Taasisi hii.

Ununuzi wa Mihtasari na Kiongozi cha Mwalimu utafanywa moja kwa moja
kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania kwa utaratibu wa "Single Source" na
hali hii imesababishwa na sababu zilizotajwa katika 2.1 hapo juu.