Aidha michango na sherehe hizi zimekuwa mzigo mkubwa sana kwa baadhi ya watu, ikiwa ni pamoja na wale wenye kipato kidogo wanaochangiwa na kulazimika kulipa michango hiyo kwa miaka mingi. Je, wajua kuwa kuna familia ambazo zimefikia kulazimisha ndugu wauze mashamba au mifugo mtaji ili kupata fedha za kuchangia sherehe?.
Je, wajua kuwa kuna watu ambao zaidi ya nusu ya kipato chao wanatumia kuchangia sherehe na huku wakishindwa kulipia huduma muhimu kama shule, matibabu, lishe, nk. Na kuwa wakati mwingine wewe au mimi (au wengine kama mimi na wewe) ndio wenyeviti na makatibu wa sherehe hiyo?. Na ni sisi tunaoona fahari ya kutumia milioni 30 au zaidi kwenye sherehe usiku mmoja?
Kuna kijana mmoja jamaa yetu juzi juzi alipata shule Australia akawa anatafuta mchango wa dola 5,000 aende. Alipata 2,000 na amwekwama kwenda. Mwaka kesho akisema anaoa tutamchangia milioni 15-20!!!.
Hii si hadithi, ni ukweli, na ni kielelezo cha ulimbukeni tuliofikia.
Siku za karibuni nimetambua kuwa kuna kundi kubwa tu linasikitishwa na huu mwenendo, na hata kutambua kuwa tunaweza kuwa tunaandikiwa dhambi kubwa (na hukumu yatusubiri) kwa jinsi wengi wetu tunashindwa kusaidia mambo ya msingi lakini tunakuwa wepesi kutoa kwenye sherehe.
Wengi wanaamini kuwa tumeshatumbukia kwenye lindi la mazoea ambapo hatuwezi kujitoa mpaka upepo uje ubadilike wenyewe!.
Mimi nafikiri wasomi tuna jukumu muhimu la kuwa chachu ya mabadiliko pale ambapo mazoea yenye madhara yanavuka mipaka na kuweza hata kuwa chanzo cha ufukara na kuviza maendeleo.
Ili kubadilisha hili jambo, lazima tuanzie mahali. Mimi napendeleza na kuanza kutekeleza. Kuanzia Januari 2011, nitapunguza michango ninayotoa. Nitatoa tu kwa mtu wa karibu sana, na nitachanga kidogo.
Usishangae nikakuchangia 20,000/= kama ulitegemea 50,000/= kwa mfano. Kuanzia July 2011, nitaacha kabisa kuchangia sherehe. Badala yake nitakuwa nachangia elimu pale ambapo mzazi hayupo au mhusika kweli hana uwezo na pia nitachangia miradi mingine ya jamii na maendeleo.
Je waniunga mkono?