Monday, September 12, 2011

BAHARIA ASIMULIA AJALI ya MV Spice Islander

     

Katika mazungumzo yake na MTANZANIA    katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, ZanzĂ­bar jana   baharia huyo alisema abiria wengi walikufa  kutokana na uzembe.

Baharia huyo aliyelazwa hospitalini hapo, alisema   iwapo kama waokoaji wangewasili mapema eneo la tukio baada ya kupata taarifa, abiria wengi wangeokolewa kwa kuwa ulikuwa na sababu za kuwaokoa, "Ajali ni ajali, lakini kwa hii ya kwetu nasema wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya uzembe wa wahusika... "Lakini, hayo tuyaache  kwa sababu yameshatokea, nakumbuka wakati  tunatoka Dar es Salaam tumbo lilikuwa likiniuma, kwa hiyo, muda mwingi nilikuwa nimelala chumbani kwetu... Ilipotimia kama saa 7.00 usiku, Bubu mmoja ambaye ni mfanyakazi wenzetu alikuja chumbani kwetu na kutuonyesha kwa ishara, kwamba tutoke nje hali imeharibika, tukamuuliza kuna nini  akazidi kutwambia tokeni nje, tulipoona anazidi kutusisitizia  tukatoka nje... Nilipofika nje tu, nikakuta maji yameanza kujaa melini, mimi na wenzangu tukaanza kuyatoa kwa ndoo na mashine za pampu.

"Baadaye umeme ukazimika na mashine zikashindwa kufanya kazi.  Sasa tukaendelea kuyatoa kwa ndoo, lakini hatukuweza lolote kwa sababu yalikuwa yakiingia kwa kasi sana... Tulipoona hivyo tukaambizana kwamba hali ni mbaya, nikawaambia wenzagu tumwambie kapteni (nahodha) awatangazie abiria. Tulipomwambia kapteni akakubali akatangaza kwamba hali ni mbaya kwa hiyo, abiria wote wawe waangalifu wakati taratibu nyingine zikifuatwa," alisema Rashid.   

Kwa mujibu wa baharia huyo, baada ya tangazo hilo, abiria walihamaki na kuanza kukimbia ovyo   kuokoa maisha yao huku wakipiga kelele za kuomba msaada.
 
"Tangazo hilo liliwatisha abiria na wakati huo maji yalikuwa yakizidi kuingia ndani, nilipoona hivyo, nikachukua 'my life jacket' (makoti ya kuogelea) nikawa nawavisha abiria mmoja baada ya mwingine na kumtupa majini... Nilifanya kazi hiyo kwa muda kidogo, baadaye nilipoona maji yamezidi nikaamua kujitosa baharini baada ya kuvaa life jacket... Nilipojitosa majini, kuna abiria walikuwa wakijirusha majini na kuniangukia, kwa hiyo, nikaamua kulivua lile life jacket ili niwe huru kuongelea na kuwaokoa wengine... Nilipokuwa majini nilishtuka kuona watu wamezagaa majini na wengine wamekufa, kwa hiyo, nilichokuwa nikifanya nilikuwa nikizivua life jacket zilizokuwa katika maiti na kuwavalisha wengine ambao nilikuwa nikiwaweka katika turubai moja ambalo ni maalumu kwa ajili ya uokoaji.

"Wakati nikiwa katika turubai hilo, kuna abiria walikuwa jirani kabisa na mahali ilipokuwa meli, nikawaambia ondokeni hapo, meli itawapindukia, wakabisha na mwishowe kweli iliwafunika kwa sababu wakati nawaambia nilikuwa nikiiona imeshaanza kuegemea upande mmoja," alisema Rashid na kulengwa na machozi na kuongeza:

"Nilipoona wenzangu wamefunikwa, niliumia sana  lakini nikasema hiyo ni mipango ya Mungu.  Baada ya hatua hiyo nikamuona mzee mmoja akiwa na mtoto wake amembeba mgongoni, akaniomba, akasema mwanangu naomba umuokoe mwanangu, nikakubali, nikamwambia mzee tulia.

'Nikamchukua yule mtoto nikampeleka katika lile turubai nilikokuwa nimewaweka wengine.

"Nilipomuokoa huyo mtoto, mbele yangu nikaona watu watatu wanalalamika, pembeni kulikuwa na mwanamke mmoja akilia kwa huruma.

"Nikamfuata huyo mwanamke, nikamkuta na kitu kama mkeka hivi amekishika, nikamwambia achia huo mkeka, akakataa akasema nitakufa, nikamzaba kibao usoni kwa nguvu, akaachia ule mkeka, nikamkamata na kumpeleka kwenye lile turubai... Baadaye nguvu zilianza kuniishia, nikawa nashuhudia kabisa wenzagu waliokuwa pembeni na sisi wakiwa wanapoteza maisha mmoja baada ya mwingine, yaani niliumia sana na nadhani hili tukio litachukua miaka mingi sana kunitoka kichwani.

"Katika lile turubai nilikuwa na abiria kama 15 niliokuwa nimewaokoa, baadaye nikaona wanaanza kuchoka kwa njaa, nikaamua kujitosa tena majini nikaanza kukusanya juice za Azam zilizokuwa zimetapakaa majini... "Nilipopata za kutosha nikaanza kuwanywesha wale abiria   wapate nguvu na kila aliyekuwa akinywa fumba moja namkataza namnywesha mwingine," alisema.

Pamoja na hatari ya kifo aliyokuwa akiiona mbele yake, baharia huyo alisema alikuwa akiwapa moyo wenzake kwa kuwaambia kuwa mahali walipokuwa palikuwa salama na hakukuwa sababu ya kuhofia maisha yao.

"Nilikuwa nawapa matumaini nikawa nawaambia tutapona tu hata kama tutapeperushwa na upepo hadi Tanga au Mombasa, lazima tutaokolewa. Ilipotimia kama saa 12.00 alfajiri, niliona helkopta kwa mbali, nikamwambia mfanyakazi mwenzagu anaitwa Almada, achukue taa moja hivi, akaichukua  akainyanyua   kuwaonyeshea wale wenye helkopta waweze kutuona, lakini hawakutuona kwa sababu walikuwa mbali ingawa sisi tulikuwa tunaiona hiyo helkopta. Nilipoona hawatuoni, nikamwambia tunyooshe bendera, alipoinyoosha wakati huo helkopta ilikuwa imekaribia ndipo wakatuona na  kutufuata huku meli za uokoaji kama Sea Bus na Sea Express zilizokuwa zikiongozana na hiyo helkopta zikatufuata na kutuokoa.

"Lakini, nakwambia kuna uzembe umefanyika… kama waokoaji wangefika mapema watu wasingekufa kwa kiasi hiki kwa sababu baada ya meli kuanza kupoteza mwelekeo, tulipiga simu polisi na bandarini kuomba msaada, lakini hawakufika hadi saa 12.00, sasa hapa tumlaumu nani, serikali au nani?  Mungu anajua,' alisema.