Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
HIVI karibuni Watanzania tulipokea habari njema lakini zenye huzuni ndani yake; kuwa kampuni ya BAE System ya Uingereza imeamuliwa na Mahakama moja ya nchi hiyo iturudishie Watanzania Dola milioni 28 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 72. Kwamba turudishiwe kwa vile rada ambayo kampuni hiyo ilituuzia haikuwa ya gharama hiyo.
Ndio, Watanzania tuliuziwa mbuzi kwenye gunia au? Na kuna mjadala unaendelea, kuwa ni kwa namna gani fedha tunazorudishiwa zitatumika. Serikali inazitaka, na kuna wanaojenga hoja fedha hizo zigawanywe kwa asasi zisizo za Kiserikali.
Ninachokiona hapa ni jinsi tunavyozama kujadili matumizi ya fedha hizo badala ya kujadili pia hali iliyolipelekea taifa letu kwenye aibu kubwa ya baadhi ya watendaji wetu, inavyoonekana, kukubali kupokea teni pasenti na kukubali nchi yetu iuziwe rada ya gharama ya chini lakini kwa bei ya juu.
Ndugu zangu,
Tuna lazima ya kujadili mfumo uliotufikisha hapa ikiwemo kuona ni kwa namna gani tunawawajibisha wale waliotufikisha kwenye aibu hii. Maana, ilipata hata kuripotiwa, kuwa aliyekuwa Waziri wa Miundo Mbinu, Andrew Chenge, alituhumiwa kuwa na dola za Kimarekani milioni moja kwenye akaunti yake huko Marekani. Habari hii ilitushtua Watanzania wengi. Wakati ule tukaambiwa, kuwa hata Ikulu ilishtuka.
Na aliyekuwa Waziri anayeshughulikia na Utawala Bora mama Sophia Simba naye alikaririwa akishangaa na hata kutamka; " Labda ameuza ng'ombe wake wote!". Yumkini Mama Simba na Chenge wana utani wa kikabila, maana sisi hatujui Waziri Chenge alikuwa na mazizi mangapi ya ng'ombe.
Lakini je, inatosha kushtuka tu bila kuchukua hatua? Tukubali, kuwa kashfa ya manunuzi ya rada ni moja ya kashfa nzito kwa Serikali na taifa kupata kutokea. Ni jambo la aibu kwa nchi. Tumeshtuka kwa kuona kichuguu. Je, kuna watakaozimia wakiona mlima wenyewe? Kama kawaida wahusika wameendelea na wataendelea kujikung'uta kama kuku waliomwagiwa maji na kuendelea na shughuli zao kama vile hakuna kilichotokea. Si tunaona? Leo tunazungumzia tutakavyotumia fedha yetu tuliorudishiwa. Hatuwazungumzii waliotufikisha kwenye aibu hii.
Maana kashfa hii inahusu tuhuma za kupokea rushwa katika manunuzi ya rada. Ni miaka nane sasa imepita tangu ununuzi huo upigiwe kelele. Hoja ilikuwa ni gharama ya juu ya rada hiyo wakati kulikuwa na rada nyingine zenye ubora unaohitajika kwa gharama nafuu.
Ni yale yale, ' The end justify the means'- kwamba hatma ya jambo ndio inayohalalisha njia za kutumia.
Anayeona kuna maslahi binafsi mbele, yuko tayari nchi iingie gharama kubwa ili mradi ameahidiwa 'teni pasenti' yake ya uhakika. Na katika hili, baadhi ya viongozi wetu hawana huruma na sisi. Hufika mahali raia tukaambiwa kwa kejeli; " Hata ikibidi mle nyasi....!". Kwamba kuna baadhi ya maamuzi yasiyo ya kimaslahi kwa umma yanatekelezwa kwa lazima kwa vile ndani yake yana maslahi binafsi kwa kundi dogo la wajanja ambao kimsingi ni wahalifu.
Katika hili ilifika mahali Serikali yetu na hususan wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ilitetea bei kubwa ya ununuzi wa rada na kuwashangaa wanaotuonea huruma nje ya mipaka yetu! Baadhi yetu tunakumbuka pale Waheshimiwa wabunge wa Bunge la Uingereza wakiongozwa na mbunge wa kujitegemea Clare Short, walipoichachafya serikali ya Bw. Tony Blair juu ya sakata la nchi yetu kuuziwa rada ya bei juu na pia rushwa kutumika katika ununuzi huo.
Itakumbukwa, Bi. Clare Short alikuwa Waziri mwandamizi wa Masuala ya Maendeleo na Misaada katika Baraza la Mawaziri la Bw. Tony Blair. Bi. Clare Short na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Kansela Gordon Brown walipinga vikali ununuzi huo. Wawili hawa, Clare na Gordon Brown walionyesha msimamo wao huo baada ya ukweli kuanza kujitokeza juu ya sakata hilo. Wabunge wale wa Uingereza walikiona kitendo cha kampuni ya BAE ya nchini Uingereza ' kutuuzia mbuzi kwenye gunia' kuwa ni kitendo cha aibu na kisicho cha ubinadamu kwa kuangalia hali za masikini wengi wa nchi kama Tanzania. Kwamba hiyo ilikuwa ni aibu kwa Uingereza.
Lakini, aibu hii kamwe haiwezi kuwa ya Uingereza tu, ni aibu yetu Watanzania. Ni aibu yetu kwa vile kuna baadhi ya Watanzania wenzetu wanatuhumiwa kuhusika na uhalifu huu.
Ikumbukwe, kuwa wakati mjadala wa ununuzi wa rada hiyo ulipofukuta mwaka ule wa 2001, sio tu baadhi yetu tulionekana wajinga kwa kuhoji ununuzi ule, bali hata wale waliokuwa nasi katika kupigania kufutiwa ama kupunguzwa kwa madeni yetu tuliwageuka; mfano mzuri ni Shirika la Oxfam.
Hao tuliwaacha wakiduwaa , wakati wao walisisitiza, kuwa Serikali ya Uingereza isitoe leseni kwa kampuni ya BAE, kwa vile mkataba huo haukuwa na manufaa kwa Watanzania walio wengi, serikali yetu wakati ule wa Mzee Mkapa, ilitamka kuupokea uamuzi wa serikali ya Uingereza 'kwa mikono miwili'. Kumbe, leo ukweli unadhihiri, mikono ya kupokea haikuwa miwili, ilikuwa mingi tu!
Ndugu zangu,
Kashfa ya manunuzi ya rada isiishie kwenye kujadili namna tutakavyoitumia ' chenji' tuliorudishiwa na kampuni ya BAE. Iwe chachu ya kujadili suala zima la maadili ya viongozi wetu. Na wale viongozi waliohusika na kashfa hii watajwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Na kwa vile manunuzi ya ' kiini macho' ya namna hiyo yamefanywa na viongozi wetu, basi, yumkini kuna mengine yenye kufanana na hayo. Tuyatafute. Nahitimisha.
0712 95 61 31 / 0788 111 765/ 0754 678 252